Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu hatari ya njaa katika nchi 16
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) zimeonya kuhusu mgogoro mkubwa wa ukosefu wa usalama wa chakula unaozidi kuwa mbaya katika nchi 16, na kuweka hatarini maisha ya mamilioni ya watu, hasa katika maeneo yenye migogoro na majanga ya hali ya hewa.
Ripoti ya pamoja yenye kichwa "Hunger Hotspots" imesema kwamba nchi sita zinakabiliwa na hatari ya njaa au janga la njaa ambazo ni Sudan, Palestina, Sudan Kusini, Mali, Haiti na Yemen, ikieleza kwamba baadhi ya jamii katika nchi hizo "zinaweza kufikia hatua ya kutumbukia kwenye baa la njaa au karibu na njaa."
Ripoti hiyo imeongeza kuwa nchi nyingine zinakabiliwa na kuzorota sana usalama wa chakula, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Nigeria, Myanmar, Somalia, Syria na Afghanistan, Burkina Faso, Chad na Kenya, pamoja na wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Cindy McCain ameeleza kwamba njaa "sio kadari isiyoweza kuepukika," akisisitiza kwamba jamii ya kimataifa ina "zana na maarifa ya kuizuia, lakini kinachokosekana ni rasilimali na nia ya kisiasa ya kuchukua hatua mara moja."
Ameongeza kuwa watoto ndio kundi lililo hatarini zaidi, kwa sababu utapiamlo hudhoofisha kinga yao ya mwili na kuongeza hatari ya magonjwa na kifo.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa migogoro na machafuko vinasalia kuwa vichocheo vikuu vya njaa katika maeneo 14 kati ya 16 yenye njaa duniani, huku mitikisiko na udhaifu wa kiuchumi na kupanda kwa bei vikizidisha mgogoro huo.
Cindy McCain pia amesema kwamba hali mbaya ya hewa kama vile mafuriko, ukame na vimbunga vinavyohusiana na "La Niña", pamoja na kupungua kwa misaada ya kibinadamu na ukosefu wa ufadhili, yote yamechangia kuenea kwa njaa.
Wakati huo huo, Qu Dongyu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) amesema: "Migogoro inasalia kuwa kichocheo kikuu cha njaa, lakini matukio ya hali ya hewa na kukosekana utulivu wa kiuchumi vinazidisha mgogoro huo.