Utafiti: Uislamu ndiyo dini inayokuwa kwa kasi zaidi duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i13447-utafiti_uislamu_ndiyo_dini_inayokuwa_kwa_kasi_zaidi_duniani
Utafiti uliofanywa na kituo cha utafiti cha Pew Research Center cha Marekani umeonyesha kuwa, Uislamu utasalia kuwa dini yenye kukuwa kwa kasi zaidi duniani katika kipindi cha miongo kadhaa ijayo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 17, 2016 14:06 UTC
  • Utafiti: Uislamu ndiyo dini inayokuwa kwa kasi zaidi duniani

Utafiti uliofanywa na kituo cha utafiti cha Pew Research Center cha Marekani umeonyesha kuwa, Uislamu utasalia kuwa dini yenye kukuwa kwa kasi zaidi duniani katika kipindi cha miongo kadhaa ijayo.

Shirika la Bloomberg limeripoti kuwa, utafiti wa kituo cha Pew chenye makao makuu yake mjini Washington umebainisha kuwa, idadi kubwa ya watu wanavutiwa na Uislamu kutokana na mafundisho yake, haswa kuhusu miamala na bishara za halali. Utafiti huo umesema kuwa, idadi kubwa ya watu wanavutiwa na namna Uislamu unavyofundisha juu ya kupata kipato cha halali na kujihusisha na biashara na uwekezaji unaofuata sheria na mafundisho ya Qurani tukufu.

Matajiri wengi wanavutiwa na uwekezaji kwa mfumo wa Kiislamu

Aidha utafiti huo umebainisha kuwa, Waislamu ndio watu tajiri zaidi duniani, wakiwa na utajiri wa takriban dola trilioni 11.5, jambo ambalo limewafanya wajasiriamali na wafanyabiashara wengi ambao sio Waislamu kutaka kuwekeza kwa mujibu wa sheria za dini hiyo.

Utafiti huu umetolewa mwezi mmoja baada ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kubainisha kuwa Uislamu ndio dini ya amani zaidi duniani. Aidha mwezi uliopita wa Julai, Robert Meggy, Mkuu wa Idara ya Habari na Utekelezaji ya Taasisi ya Kimataifa kwa Ajili ya Amani alisema kuwa, Uislamu hauna mfungamano wa aina yoyote na mashambulizi wala vitendo vya kigaidi ambavyo vimekuwa vikifanywa kwa jina la dini hiyo, kwa sababu magaidi ni watu wasio na dini.

Uislamu dini ya amani

Licha ya propaganda chafu dhidi ya Uislamu lakini idadi ya watu wanaosilimu na kuingia katika dini hiyo tukufu imekuwa ikiongezeka kwa kasi mno duniani hususan katika ulimwengu wa Magharibi.