Rais Putin: Russia itaendelea kuwa rafiki na mshirika wa Iran
-
Rais Vladimir Putin
Rais wa Russia amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kuwa mshirika mwaminifu wa Iran katika nyakati hizi ngumu za kukabiliana na hujuma ya kichokozi ya utawala wa Kizayuni na Marekani
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Ikulu ya Kremlin imetangaza kuwa Rais Vladimir Putin wa Russia ametuma ujumbe wa pongezi za Nowruz kwa Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, pamoja na Masoud Pezeshkian, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Nowruz ni sherehe inayoashiria mwanzo wa mwaka mpya wa Kiirani, ambao mwaka huu umeanza tarehe 21 Machi na kuadhimisha kuingia mwaka wa 1405.
Katika jumbe hizi tofauti, Rais Putin amesisitiza kuwa Russia itaendelea kuwa rafiki na mshirika wa Iran
Rais wa Russia pia amewatakia watu wa Iran kufikia mwisho wenye heshima katika majaribu haya magumu, na akasisitiza kuwa Russia itaendelea kuwa rafiki mwaminifu na mshirika wa kuaminika wa Iran katika nyakati hizi zenye changamoto.
Putin awapongeza Waislamu wa Russia
Wakati huo huo, siku ya Ijumaa, Rais Putin katika ujumbe wa kuwapongeza Waislamu wa nchi hiyo kwa sikukuu ya Eid al‑Fitr, alisifu mchango chanya wa jamii ya Kiislamu nchini Russia. Putin amesema: “Eid al‑Fitr, mwishoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwa karne nyingi imekuwa ikiakisi maadili ya waumini ya kujiboresha kimaadili, rehema, huruma, na kurejea kwenye tunu za kudumu za Uislamu.”
Rais wa Russia amebainisha pia kwamba taasisi na mashirika ya Kiislamu nchini humo yanatoa mchango muhimu katika kuimarisha taasisi ya familia, kulea na kuelimisha vijana, kuendeleza mazungumzo yenye kujenga na taasisi za serikali na za kijamii, pamoja na kujitolea bila kuchoka katika utekelezaji wa mipango ya kizalendo, kielimu na kibinadamu.