Mgogoro wa nishati waiathiri Ulaya; Slovenia mafuta yanatolewa kwa mgao
https://parstoday.ir/sw/news/world-i137552-mgogoro_wa_nishati_waiathiri_ulaya_slovenia_mafuta_yanatolewa_kwa_mgao
Athari mbaya za vita vya Marekani na utawala ghasibu wa Israel zinaanza koenekana waziwazi barani Ulaya na kuathiri sekta mbalimbali za viwanda, usafirishaji na maisha ya watu wa kawaida.
(last modified 2026-03-24T07:40:08+00:00 )
Mar 24, 2026 07:40 UTC
  • Mafuta ya petroli yanza kutolewa kwa ngao Ulaya
    Mafuta ya petroli yanza kutolewa kwa ngao Ulaya

Athari mbaya za vita vya Marekani na utawala ghasibu wa Israel zinaanza koenekana waziwazi barani Ulaya na kuathiri sekta mbalimbali za viwanda, usafirishaji na maisha ya watu wa kawaida.

Slovenia imetajwa kuwa nchi ya kwanza mwanachama wa Umoja wa Ulaya kuanza kutoa mafuta ya petroli kwa mgao ili kukabiliana na athari mbaya za vita vilivyo kinume na sheria vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ripoti zinasema, kupanda bei ya mafuta ya petroli nchini Slovenia kumepelekea kujitokeza kinachoitwa “utalii wa mafuta”, kwa maana kwamba raia wa nchi hiyo sasa wanasafiri kwenda nchi jirani kama Austria kwa ajili ya kupata nishati za petroli na dizeli kwa bei nafuu.

Kwa mujibu wa taratibu mpya zilizowekwa nchini Slovenia, madereva wa magari ya binafsi hawaruhusiwa kununua zaidi ya lita 50 za nishati kwa siku.

Kutokana na mashambulizi ya kijeshi ya Marekni na Israel dhidi ya Iran, usafirishaji wa meli kubwa za mafuta kupitia Lango Bahari la Hormuz, ambayo ni njia muhimu sana ya kimataifa, umekumbwa na matatizo makubwa, jambo ambalo limepelekea kupanda sana bei ya nishati katika masoko ya kimataifa.

Kupanda bei ya nishati kumezidisha wasiwasi mkubwa kote duniani na kuzilazimisha nchi za Magharibi kuchukua hatua za dharura za kudhibiti bei na mgao wa bidhaa hiyo.

Wakati huo huo Wakala wa Kimataifa wa Nishati umetangaza kuwa, nchi wanachama zimechukua hatua ya kuingiza karibu mapipa milioni 400 ya mafuta ya akiba yao ya dharura masokoni. Hatua hiyo imetajwa kuwa ndiyo kubwa zaidi ya kuingizwa sokoni mafuta ya dharura ya akiba katika historia ya shirika hilo.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa kupanda bei ya nishati kwa kawaida hupelekea kupanda bei ya usafirishaji, gharama za chakula na kuongezeka bili za wananchi za kulipia umeme, gesi na nishati kwa ujumla.