Trump: NATO ni simbamarara wa karatasi, ninafikiria kujiondoa kwenye shirika hili
-
Donald Trump
Rais wa Marekani amesema kwamba Washington inafikiria kwa dhati kujiondoa kwenye Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi (NATO).
Akizungumzia msimamo wa NATO wa kukataa kushiriki katika vita vyake dhidi ya Iran na kutuma majeshi katika Lango Bahari la Hormuz, Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba suala la kujiondoa Marekani kwenye muungano huo wa kijeshi wa nchi za Magharibi limepita kiwango cha kuangaliwa upya. “Sijawahi kushawishiwa na NATO. Siku zote nilijua walikuwa simbamarara wa karatasi, na Putin (Rais wa Russia) anajua hilo pia," amesema Donald Trump.
Rais wa Marekani amedai kwamba: "Siku zote tumekuwa huko, hata Ukraine. Ukraine haikuwa tatizo letu. Huo ulikuwa mtihani na tulijitokeza kwa ajili yao na tumejitokeza wakati wote. Lakini hawakujitokeza kwa ajili yetu."
Donald Trump ameendelea kwa kumkosoa Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer kwa kukataa kuingia katika vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na kuhoji nguvu ya jeshi la majini la nchi hiyo. "Hata hamna jeshi la majini," amesema Trump na kuongeza. "Manowari zenu za kubeba ndege hazifanyi kazi na zimechakaa sana."
Wakati huo huo, Alice Ruffo, Waziri wa Nchi wa Majeshi ya Ufaransa, amejibu ukosoaji wa Trump dhidi ya NATO kwa kutojiunga na uchokozi wa Marekani dhidi ya Iran, akisema: "NATO ni muungano wa kijeshi unaohusika na usalama wa eneo la Euro-Atlantic na haipaswi kufanya operesheni katika Mlango-Bahari wa Hormuz jambo ambalo ni kinyume na sheria za kimataifa."