Polisi ya Scotland, Uingereza, yapasisha vazi la Hijab
Polisi ya Scotland Yard ya nchini Uingereza imepasisha vazi la staha ya mwanamke wa Kiislamu, Hijabu kama njia ya kuwavutia Waislamu kujiunga na jeshi hilo.
Jeshi hilo limesema, vazi la Hijab ni uamuzi wa mtu binafsi, hivyo linakubaliana na suala la kuwa sare rasmi ya jeshi hilo.
Mkuu wa jeshi la polisi la Scotland, Phil Gormley alitangaza habari hiyo jana Jumatano na kusema kuwa, ana furaha kuona kwamba, hatua hiyo imeungwa mkono na kupokewa vizuri na jamii za Waislamu wa Uingereza pamoja na maafisa wa polisi na wafanyakazi wengine wa jeshi hilo.

Aidha amesema, hatua hiyo imepokewa vizuri pia na Jumuiya ya Polisi Waislamu SPMA ambayo iliundwa mwaka 2010 na ina uhusiano mzuri na wa karibu na jumuiya mbalimbali za Waislamu nchini Uingereza.
Fahad Bashir, mkuu wa Jumuiya ya Polisi Waislamu SPMA huko Scotland amesema kuwa, hiyo ni hatua nzuri kuelekea kwenye njia sahihi na kwamba sasa wasichana na wanawake wengi Waislamu watavutika kujiunga na jeshi hilo kwani hawatakuwa tena na kizuizi vya mavazi.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Telegraph la nchini Uingereza, katika mwaka wa fedha wa 2015-2016 polisi ya Scotland imepokea maombi elfu nne na 809 ya makuruta wanaotaka kujiunga na jeshi hilo ambapo maombi 127 kati yake yametoka kwa watu wa jamii za wachache wakiwemo Waislamu.