Kongamano kubwa la Waislamu lafanyika katika jimbo la Chicago, Marekani
Kongamano kubwa la 53 la Jamii ya Kiislamu ya Amerika ya Kaskazini (ISNA) linafanyika katika jimbo la Chicago nchini Marekani.
Kongamano hilo la kila mwaka lililoanza siku ya Ijumaa linaendelea kwa muda wa siku nne na linatazamiwa kumalizika leo Jumatatu.
Kauli mbiu ya kongamano hilo kwa mwaka huu ni "Nukta Muhimu: Kuongoza Changamoto na Kutumia Fursa".
Rais wa Jamii ya Kiislamu ya Amerika ya Kaskazini Azhar Azzez amesema ISNA ndiyo jumuiya kongwe zaidi na kubwa zaidi ya Kiislamu katika Amerika ya Kaskazini. Ameongeza kuwa jumuiya hiyo inakuza maendeleo ya jamii ya Kiislamu kupitia mikutano, makongamano, majukwaa ya kielimu, programu za vijana, shughuli za kijamii na harakati baina ya wafuasi wa dini tofauti.
Kuhusu jinsi ya kukabiliana na kampeni chafu za kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu Azeez amesema, jumuiya ya Jamii ya Kiislamu ya Amerika ya Kaskazini inalenga kuunganisha watu wa imani na asili tofauti kwa moyo wa kuleta amani na mafahamiano zaidi.
Siku ya Jumamosi na Jumapili yamefanyika pia mashindano ya Qur'ani katika usomaji na kuhifadhi Qur'ani kwa lengo la kuwahamasisha vijana kujifunza na kukitalii kitabu hicho cha wahyi.
Shakhsia kadhaa maarufu wa Kiislamu akiwemo Dakta Tariq Ramadhan na Sheikh Hamza Yusuf wamehutubia kongamano la mwaka huu.../