Mawaziri wa Uingereza wataka nchi ibakie ndani ya EU
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema kuwa baraza lake la mawaziri limeafiki kubakia nchi yao kwenye Umoja wa Ulaya (EU) lakini kuwe na mabadiliko kwenye sheria za muungano huo.
Cameron amesema hayo leo kwenye kikao na waandishi wa habari ambapo pia amesema kura ya maamuzi itafanyika Juni 23 ambapo Waingereza wataamua endapo wanataka nchi yao iendelee kubakia kwenye Umoja wa Ulaya au la. Waziri Mkuu wa Uingereza amesema kukiwa na mabadiliko ya ki msingi katika uendeshaji wa mambo ndani ya EU, nchi yake itakuwa salama zaidi na yenye nguvu kisiasa na kiuchumi. Hata hivyo David Cameron amesisitiza kuwa London haitakubali kuwa sehemu ya EU katika mazingira ya sasa hivi. Katika siku za hivi karibuni Waziri Mkuu huyo wa Uingereza amekuwa akifanya safari za hapa na pale katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kujaribu kuwashawishi viongozi wa muungano huo kukubali mabadiliko yafanyike ndani ya jumuiya hiyo ili kuepusha uwezekano wa London kujiondoa.