Deby: EU ishirikiane na viongozi wa Afrika kukomesha wimbi la wahajiri
Rais Idris Deby wa Chad amesema ili kulipatia ufumbuzi jinamizi la wahajiri kumiminika barani Ulaya, sharti Umoja wa Ulaya uwahusishe viongozi wa Afrika katika mikakati yake ya kukomesha wimbi hilo la wahamiaji haramu.
Rais Deby aliyasema hayo jana Jumatano katika mkutano wake na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel mjini Berlin na kuongeza kuwa, kuna haja kwa EU kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa kundi la G5, linalozijumuisha nchi 5 za Jangwa la Sahel, kuhusu kadhia hiyo ya wimbi la wahajiri.
Amesema iwapo taasisi hizo mbili (G5 na EU) zitashirikiana na kufanya kazi bega kwa bega, mbali na kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu kutoka eneo la Sahel, changamoto nyinginezo kama za ugaidi, ulanguzi wa mihadarati na biashara ya utumwa mambo leo zinaweza kupatiwa ufumbuzi.
Merkel kwa upande wake ametoa wito wa kuzidishwa misaada ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya ustawi wa nchi za Afrika ili kukomesha wimbi la wahamiaji haramu wa bara hilo kuelekea Ulaya na kusisitiza kuwa Ujerumani itatoa kipaumbele kwa suala la wahajiri kutoka Afrika katika mkutano wa mwaka ujao wa nchi za kundi la G20.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR zinasema, hadi kufikia katikati ya mwezi Juni mwaka huu, karibu wahamiaji haramu elfu 50 kutoka nchi za Kiafrika waliwasili kwa boti barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranean na kwamba kufikia mwishoni mwa mwaka ujao, bara hilo litakuwa limepokea zaidi wa wahajiri milioni moja na laki nne.