Kushadidi tuhuma baina ya Trump na Clinton, kuelekea uchaguzi Marekani
Ushindani katika kampeni za urais nchini Marekani umeshika kasi ikiwa ni siku chache zimesalia kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais nchini humo.
Hivi sasa Donald Trump na Hillary Clinton, wagombea wa vyama vya Republican na Democrat, wanajitahidi kila mmoja katika siku 12 zilizosalia kuweza kuwavutia wananchi kwenda kwenye masanduku ya kupigia kura kwa maslahi yake. Katika fremu hiyo, Trump ameutaja uchaguzi wa mwaka huu kuwa ni fursa ya mwisho kwa ajili ya kuwaokoa Wamarekani.
Kwa upande wake Hillary Clinton amemtaja Donald Trump kuwa tishio kwa demokrasia nchini Marekani. Hii ni katika hali ambayo, kwa mujibu wa utamaduni wa kisiasa na uchaguzi nchini Marekani, daima wagombea au vyama shindani, huwa vikikosoa siasa na mipango ya upande wa pili. Hii ni katika hali ambayo katika uchaguzi wa mwaka huu, msingi na mfumo wa kisiasa na mustakbali wa taifa hilo, vimekuwa ndio changamoto kuu. Kwa upande mmoja, Trump ameutaja ushindi wake katika uchaguzi ujao kuwa njia pekee ya kuiokoa Marekani kutokana na hali mbaya inayoikabili hivi sasa nchi hiyo. Kwa mtazamo wa mwanasiasa huyo njia hiyo ndio inayoweza kuwavutia wapigakura ambao aghlabu yao ni watu ambao hawana imani na mfumo mzima wa siasa na wanasiasa wa sasa wa nchi hiyo, huku wakiwa hawana nia ya kushiriki katika uchaguzi, kuweza kumchagua yeye.
Kwa mtazamo wa waungaji mkono wa Donald Trump, kuongezeka kwa watu wanaopinga mfumo wa uchaguzi, ndiko kunakompa mgombea wa chama cha Republican nafasi zaidi ya kushinda. Kinyume chake, Hillary Clinton sambamba na kutetea mfumo uliopo wa kisiasa na kiuchumi nchini Marekani, anafanya juhudi zaidi za kumuarifisha hasimu wake kuwa si tu kwamba ni tishio kwa chama chake cha Democrat, bali ni hatari pia kwa demokrasia ya taifa zima. Clinton ameelekeza kampeni zake kwa wapigakura ambao aghlabu yao hawashiriki kwenye uchaguzi kutokana na wao kutojali au kukosa imani na mfumo wa kisiasa unaotawala hivi sasa nchini humo.
Kwa ajili hiyo, waungaji mkono wa Hillary Clinton, wanataraji kwamba sambamba na kupiga kengele ya hatari kwa mfumo wa demokrasia nchini, waweze pia kuunda vuguvugu la kijamii dhidi ya mgombea wa upinzani. Kwa vyovyote vile, inaonekana kuwa, kushadidi mashambulizi ya mirengo miwili nchini Marekani sanjari na kubadilika uchaguzi wa mwezi Novemba kuwa kadhia ya uhai na kifo kwa ajili ya harakati mbili za uhafidhina na uleberali nchini Marekani, kunaonyesha uwezekano wa kuongezeka idadi washiriki wa kisiasa kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
Hata hivyo isisahaulike kuwa, pamoja na hali hiyo takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa la watu wasiojali kupiga kura, licha ya kutimiza masharti stahiki. Pamoja na hali hiyo, uchaguzi wa rais wa mwaka huu 2016 unatofautiana sana na chaguzi zilizopita. Ni kwa ajili hiyo ndio maana inatarajiwa kuongezeka kwa kiasi fulani ushiriki wa kisiasa katika uchaguzi wa mwaka huu. Pamoja na kuwepo wasi wasi mwingi juu ya usalama wa zoezi zima la uchaguzi, lakini weledi wengi wa mambo wanaamini kuwa, madai ya Donald Trump na Hillary Clinton hayawezi kutatua matatizo na changamoto nyingi zinazolikabili taifa hilo.