China: Trump asijaribu kabisa kuingilia masuala yetu ya ndani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19207-china_trump_asijaribu_kabisa_kuingilia_masuala_yetu_ya_ndani
Huku ulimwengu ukiwa bado umepatwa na mshangao kufuatia ushindi wa hapo jana wa mgombea wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump, kwa upande wake vymbo vya habari vya serikali ya Uchina, vimetoa onyo kali kwa rais huyo mteule kutothubutu kuingilia masuala yake ya ndani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2016 10:03 UTC
  • China: Trump asijaribu kabisa kuingilia masuala yetu ya ndani

Huku ulimwengu ukiwa bado umepatwa na mshangao kufuatia ushindi wa hapo jana wa mgombea wa chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump, kwa upande wake vymbo vya habari vya serikali ya Uchina, vimetoa onyo kali kwa rais huyo mteule kutothubutu kuingilia masuala yake ya ndani.

Vyombo hivyo vya habari vya serikali nchini China vimetoa onyo kali kwa Trump kwamba kamwe asithubutu kuingilia siasa za ndani za nchi hiyo. Shirika la Habari la Xinhua hii leo limeandika kuwa, Donald Trump anatakiwa kufanya juhudi kubwa za kiushirikiano kwa ajili ya kuwa na uhusiano mwema na Beijing. Nalo gazeti la Global Times ambalo ni gazeti la chama tawala nchini China limeandika kuwa, ushindi wa Trump umewashtua watu wengi duniani na kwamba mwanasiasa huyo hawezi kubadili siasa za kigeni za Marekani.

Donald Trump, rais mteule wa Marekani

Inafaa kuashiria kuwa, kwa mara kadhaa rais huyo mteule wa Marekani alikuwa akiilenga moja kwa moja China katika kampeni zake kwa kudai kuwa Beijing ndio muhusika mkubwa wa ongezeko la ukosefu wa ajira nchini Marekani na hivyo akasisitiza kuwa, endapo atachaguliwa kura rais, atazidisha ushuru wa asilimia 45 kwa bidhaa za China zinazoingizwa Marekani. China na Marekani zimekuwa zikitofautiana juu ya masuala kadhaa hususan uingiliaji wa Washington katika nchi zingine na kadhalika suala zima la uchumi.