ICC yazipigia magoti nchi za Afrika, yaziasa zisiondoke katika mahama hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19618-icc_yazipigia_magoti_nchi_za_afrika_yaziasa_zisiondoke_katika_mahama_hiyo
Maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC wamezitaka nchi za bara Afrika kutojiengua kuwa wanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 17, 2016 00:55 UTC
  • ICC yazipigia magoti nchi za Afrika, yaziasa zisiondoke katika mahama hiyo

Maafisa wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC wamezitaka nchi za bara Afrika kutojiengua kuwa wanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo.

Akizungumza jana Jumatano katika ufunguzi wa mkutano wa kila mwaka wa Jumuiya ya Nchi Wanachama wa Mktaba wa Roma mjini The Hague nchini Uholanzi, Rais wa jumuiya hiyo Sidiki Kaba ameziasa nchi za Afrika zisalie kuwa wanachama wa mahakama hiyo ya kimataifa iwapo zinaunga mkono mkondo wa haki kwa kila mtu.

Amesema katika dunia ya sasa iliyozungukwa na mizozo na jinai za kila namna, kuna udharura wa mataifa yote kuunga mkono uwepo wa haki kwa kila mtu pasina kujali hali yake ya kijamii.

Naye Zeid Ra'ad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameuambia mkutano huo kuwa: "Ingawa wenye nguvu wanashinikiza kuondoka katika mahakama hii, lakini waathirika wa ghasia na jinai za kivita pamoja na wanyonge daima wamekuwa wakitaka nchi zao zibakie kuwa wanachama wa Mkataba wa Roma wakifahamu fika kuwa, hakuna mbadala wa ICC."

Sidiki Kaba, Rais wa Jumuiya ya Nchi Wanachama wa Mktaba wa Roma

Haya yanajiri siku moja baada ya Farhan Haq, Msemaji wa Umoja wa Mataifa kutangaza kuwa Gambia itaacha rasmi kuwa mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo ya mjini The Hague nchini Uholanzi kuanzia Novemba 10 mwaka ujao 2017.

Mwezi uliopita wa Oktoba, Gambia ilijiunga na orodha ya nchi kadhaa za Afrika zilizotangaza azma yao ya kujiondoa katika Mkataba wa Roma uliobuni ICC Julai mwaka 2002.

Tayari Afrika Kusini na Burundi zimeanzisha mchakato wa kujiondoa katika Mkataba wa Roma kutokana na kile viongozi wa nchi hizo sawa na viongozi wengine wa Kiafrika wanakitaja kuwa, ICC kuwasakama tu viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi. Aidha Kenya, Uganda na Namibia zimeashiria kuwa yumkini nazo zikajiunga na mkondo huo wa kujiengua ICC.