Ufilipino kujiunga na Russia na nchi za Afrika dhidi ya ICC
Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte amesema huenda taifa lake likafuata mkondo wa Russia na kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.
Akizungumza hapo jana, alisema ICC ni chombo 'kisichokuwa na maana' kinachoendeshwa na Wamagharibi huku akiukashifu Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kushughulikia masuala nyeti kama kuzima vita na machafuko katika sehemu mbalimbali duniani.
Rais wa Ufilipino amesema nchi za Magharibi zimekuwa zikiishutumu serikali yake kwa kupambana na mihadarati zikidai kuwa maafisa wa usalama wa nchi hiyo wanatumia mkono wa chuma kuwakabili washukiwa wa mihadarati.
Jumatano iliyopita, Rais Vladimir Putin alisaini dikrii ya kiishara ya kujiengua Russia kutoka mahakama hiyo iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi, ingawa nchi hiyo sio mwanachama wa Mkataba wa Roma.
Wakati huo huo, Rais Omar al-Bashir wa Sudan amepongeza hatua hiyo ya Russia na kusema kuwa itatoa msukumo kwa nchi zaidi kujiengua huku akiitaja ICC kama mahakama iliyofeli.
Mwezi uliopita wa Oktoba, Gambia ilijiunga na orodha ya nchi kadhaa za Afrika zilizotangaza azma yao ya kujiondoa katika Mkataba wa Roma uliobuni ICC Julai mwaka 2002.
Tayari Afrika Kusini na Burundi zimeanzisha mchakato wa kujiondoa katika Mkataba wa Roma kutokana na kile viongozi wa nchi hizo sawa na viongozi wengine wa Kiafrika wanakitaja kuwa, ICC kuwasakama tu viongozi wa nchi za bara hilo, huku ikifumbia macho jinai zinazofanywa na viongozi wa Magharibi. Aidha Kenya, Uganda na Namibia zimeashiria kuwa yumkini nazo zikajiunga na mkondo huo wa kujiondoa ICC.