Hizbullah yasema Trump ni mtu mwenye chuki na ubaguzi
Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesema kuchaguliwa mwanasiasa mwenye chuki na ubaguzi nchini Marekani kwa upande mmoja; na maandamano ya nchi nzima ya kulalamikia ushindi wa bilionea huyo kwa upande mwingine, ni dhihirisho kuwa nchi hiyo iko katika mgogoro mkubwa.
Katika mahojiano na shirika la habari la Tasnim la Iran mjini Beirut, Sheikh Naim Qassim amesema sera za chuki na za kibaguzi za Trump zitawasababishia matatizo makubwa watu wengi wa Marekani na kubainisha kuwa, yumkini mwanasiasa huyo wa chama cha Republican akalegeza misimamo na kukosa kutekeleza baadhi ya ahadi zake za kibaguzi, iwapo maandamano yatashtadi zaidi.
Haya yanajiri siku chache baada ya Trump kuwateua watu wenye chuki na Uislamu kuhudumu katika Ikulu ya White House, jambo linaloashiria muendelezo wa sera zake za chuki ambazo zimewatia hofu Waislamu nchini humo.
Miongoni mwa waliyoteuliwa na Tump ni afisa mstaafu katika Jeshi la Marekani Luteni Jenenrali Michale Flynn, mwenye historia ya kutoa matamshi makali dhidi ya Uislamu pamoja na Seneta Jeff Session ambaye amekubali uteuzi wa Trump wa kuwa mwanasheria mkuu Marekani. Seneta huyo anaunga mkono kauli ya Trump ya kutaka kuzuiwa Waislamu kuingia Marekani. Aidha Trump alimteua mjumbe wa Congress, Mike Pompeo kuwa mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, ambaye amekuwa akitoa madai kuwa viongozi wa Waislamu Marekani hawachukui misimamo imara dhidi ya ugaidi.
Ijumaa iliyopita mashirika ya kijamii na viongozi wa Waislamu Marekani walitangaza bayana wasiwasi wao kuhusu hatua ya Trump kuwateua watu wenye chuki na Uislamu katika nyadhifa muhimu za usalama wa taifa.
Tangu kutangazwa mshindi Trump, Marekani imekuwa ikishuhudia maandamano katika kona mbali mbali za nchi, ya kumtaka asitekeleze baadhi ya ahadi zake kama vile za kuwatimua nchini humo wahajiri, Waislamu na Wamarekani wenye asili ya Afrika.