Mkutano wa Waislamu America waanza katika mji wa Detroit, Michigan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20263-mkutano_wa_waislamu_america_waanza_katika_mji_wa_detroit_michigan
Mkutano wa 12 wa kila mwaka wa Jumuiya ya Kiislamu ya America ya Kaskazini umeendelea leo katika mji wa Detroit kwenye jimbo la Michigan huko Marekani.
(last modified 2026-08-18T17:02:23+00:00 )
Nov 27, 2016 02:10 UTC
  • Mkutano wa Waislamu America waanza katika mji wa Detroit, Michigan

Mkutano wa 12 wa kila mwaka wa Jumuiya ya Kiislamu ya America ya Kaskazini umeendelea leo katika mji wa Detroit kwenye jimbo la Michigan huko Marekani.

Mkutano huo wa Waislamu wa America ya Kaskazini unajadili matatizo yanayoikabili jamii ya Waislamu nchini Marekani ikiwa ni pamoja na kushadidi hujuma na propaganda chafu dhidi ya dini ya Uislamu.

Miongoni mwa masuala muhimu yanayojadiliwa katika mkutano huo wa kila mwaka ni taathira mbaya za kisiasa za uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni nchini Marekani na radiamali ya jamii ya Waislamu wa nchi hiyo.

Naibu Mkurugenzi wa Ustawi wa Jumuiya ya Kiislamu ya America Kaskazini (IONA), William Antone amesema kuwa, mkutano huo pia unajidili mbinu za kubadili fikra potofu kwamba, Waislamu ni wageni katika jamii ya Marekani.

Mbali na hotuba za wataalamu wa masuala mbalimbali, mkutano huo pia unajumuisha warsha za mafundisho kuhusu masuala ya ustawi na mazungumzo.

Msikiti uliochomwa moto, Marekani

Wimbi la propaganda chafu na hujuma dhidi ya Waislamu limeongezeka zaidi nchini Marekani baada ya kuchaguliwa Donald Trump kuwa Rais wa Marekani. Katika kampeni zake za uchaguzi, rais mteule wa Marekani alikuwa akitoa matamshi ya kibaguzi dhidi ya Waislamu na alitoa wito wa kufungwa misikiti ya wafuasi wa dini hiyo nchini Marekani.