Makumi wapoteza maisha katika mtetemeko wa ardhi Indonesia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20938-makumi_wapoteza_maisha_katika_mtetemeko_wa_ardhi_indonesia
Makumi ya watu wamefariki dunia na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliolikumba eneo la kaskazini mwa Indonesia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 07, 2016 07:54 UTC
  • Makumi wapoteza maisha katika mtetemeko wa ardhi Indonesia

Makumi ya watu wamefariki dunia na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi uliolikumba eneo la kaskazini mwa Indonesia.

Zilzala hiyo yenye ukubwa 6.4 kwa kipimo cha rishta, imeutikisa mkoa wa Aceh, kaskazini mwa nchi, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 54 huku wengine zaidi ya 70 wakijeruhiwa.

Habari zinasema kuwa, yumkini idadi hiyo ikaongezeka, kutokana na kukwama watu kwenye vifusi vya majengo yaliyoporomoka kutokana na mtetemeko huo.

Sehemu ya athari za mtetemeko wa ardhi mkoani Aceh, Indonesia

Mkoa huo ambao uko kaskazini magharibi mwa kisiwa cha Sumatra, umekuwa ukishuhudia mitetemeko mingi ya ardhi. Mwaka 2013, watu zaidi ya 400 waliaga dunia katika mtetemeko mwingine wa ardhi katika mkoa huo, uliokuwa na ukumbwa wa 7.7 kwa kipimo cha rishta.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa, mwaka 2004 zilzala ya chini ya maji ilitokea katika Bahari Hindi na kusababisha Tsunami katika nchi kadhaa huku Indonesia ikiathiriwa zaidi. Watu 170,000 walifariki dunia kwenye janga hilo la kimaumbile nchini Indonesia hususan katika mkoa wa Aceh. 

Aidha makumi ya maelfu ya watu wengine waliaga dunia katika zilzala hiyo, katika nchi za Sri Lanka, India na Thailand.