Wilders apatikana na hatia ya ubaguzi dhidi ya Waislamu Uholanzi
Geert Wilders mbunge mwenye chuki dhidi ya Uislamu nchini Uholanzi amepatikana na hatia ya kuwatusi watu wenye asili ya Morocco na kuwabagua.
Kwa mujibu wa mashtaka dhidi ya Wilders, katika mkutano wa kampeni mwaka 2014 aliongoza wafuasi wake waliokuwa wakitoa nara za kutaka Wamorocco wanaoishi nchini Uholani waondoke.
Katika hukumu iliyotolewa jana Ijumaa, majaji watatu walimpata na hatia lakini hakufungwa jela kama alivyotaka mwendesha mashtaka.
Majaji hawakumuadhibu Wilders kwa madai kuwa kupatikana na hatia ni adhabu tosha. Mwendesha mashtaka wa Uholanzi ambaye alitaka Wilders atozwe faini ya Euro 5000 naye pia amesema kupatikana na hatia ni muhimu hata kuliko adhabu na hivyo ameafiki uamuzi wa majaji wa kutotoa adhabu ya kifungo cha jela wala faini kwa mwanasiasa huyo mwenye misimamo ya chuki dhidi ya Waislamu. Wilders ambaye hakuhudhuria kikao hicho cha mahakama amesema atakata rufaa kuhusu hukumu hiyo.

Baadhi ya weledi wanasema hukumu hiyo itampa msukumo Wilders ambaye anataka chama chake kinachojiita Freedom Party kipate wingi wa kura katika uchaguzi wa mwaka 2017. Chama hicho chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia, kinaendelea kupata umashuhuri nchini Uholanzi kutokana na kujikita kwenyei hisia za chuki dhidi ya wageni na Waislamu nchini humo na kote barani Ulaya.