Russia: Hatujaafikiana chochote na US kuhusu magaidi wa Aleppo
https://parstoday.ir/sw/news/world-i21259-russia_hatujaafikiana_chochote_na_us_kuhusu_magaidi_wa_aleppo
Serikali ya Russia imekanusha ripoti za kipropaganda zinazodai kuwa nchi hiyo imesaini mapatano na Marekani ya kuwapa kinga na msamaha magaidi waliosalia katika mji wa Aleppo nchini Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 12, 2016 03:48 UTC
  • Russia: Hatujaafikiana chochote na US kuhusu magaidi wa Aleppo

Serikali ya Russia imekanusha ripoti za kipropaganda zinazodai kuwa nchi hiyo imesaini mapatano na Marekani ya kuwapa kinga na msamaha magaidi waliosalia katika mji wa Aleppo nchini Syria.

Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, madai yaliyotolewa na magenge ya kigaidi mjini Aleppo yalipohojiwa na shirika la habari la Reuters kwamba Moscow na Washington zimeafikiana kuwafungulia njia za kuelekea maeneo salama wanachama waliosalia wa magenge ya kigaidi na familia zao katika mji huo, ni madai ya kubuni na yasiyokuwa na mantiki.

Hata hivyo amesema kuwa Marekani na Russia zitaendelea kufanya mazungumzo kuhusu kadhia ya Aleppo mjini Geneva na kwamba kwa sasa serikali ya Moscow inandaa mazingira ya kuwaondoa salama raia katika mji huo.

Jeshi la Syria likishika doria katika mji wa Aleppo

Katika miezi ya karibuni vikosi vya jeshi la Syria vimefanikiwa kuyazingira maeneo ya mashariki mwa mji wa Aleppo; na kutokana na mafanikio yaliyopatikana, maeneo hayo yanakaribia kukombolewa kikamilifu kutoka mikononi mwa makundi ya kitakfiri.

Aleppo au Halab imekuwa miongoni mwa ngome kuu za makundi ya kigaidi nchini Syria kwa kipindi cha zaidi ya miaka 5 sasa. Inaarifiwa kuwa, jeshi la Syria hadi sasa limeshakomboa asilimia 93 ya maeneo yaliyokuwa yakidhibitiwa na magaidi katika mji huo. 

Mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Al-Jaafari

Hii ni katika hali ambayo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni lilipitisha kwa kura 122 za 'ndiyo' na 13 za 'hapana' azimio la kuitaka serikali ya Damascus isitishe mapambano yake dhidi ya magaidi wa kitakfiri, zifunguliwe njia za kufikisha misaada ya kibinadamu nchini kote na kuhitimishwa mizingiro yote iliyowekwa ukiwemo mzingiro dhidi ya mji wa Aleppo; hatua ambayo imelaaniwa vikali na Mwakilishi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar Al-Jaafari ambaye amesisitiza kuwa, huko ni kutia kigugumizi katika mapambano dhidi ya makundi yanayobeba silaha ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.