Kundi la Daesh limetishia tena kuishambulia Russia
Kundi la kigaidi la Daesh limetuma ujumbe na kutishia kuzishambulia balozi za Russia kote ulimwenguni.
Kundi la Daesh leo Jumatano limetuma ujumbe wa sauti unaojumuisha maeneo, anwani na taarifa za kimawasiliano zinazohusiana na balozi za Russia katika maeneo mbalimbali duniani. Ujumbe wa kundi hilo la kigaidi unaeleza kuwa, balozi za Russia zilizopo Uganda, Azerbaijan, Albania na katika nchi nyingine kadhaa zitashambuliwa na kundi hilo. Andrey Karlov aliyekuwa Balozi wa Russia nchini Uturuki aliuawa kwa kupigwa risasi nane na mtu aliyetajwa kwa jina la Mevlut Mert Altintas afisa polisi wa Uturuki. Balozi huyo wa Russia alipigwa risasi wakati alipokuwa akihutubia katika maenyesho ya sanaa ya picha huko Ankara.
Balozi na balozi ndogo za Russia katika maeneo mbalimbali duniani zimewekwa katika hali ya tahadhari kwa kuimarishwa usalama wazo baada ya kuawa balozi wa nchi hiyo mjini Ankara hapo juzi. Askari maalumu wa Uturuki walifanikiwa kumuuwa muuaji huyo baada ya kulizingira eneo la maeonyesho.