Pew: Waislamu wahanga wa ugaidi nchini Marekani
Matokeo ya uchunguzi mpya wa maoni uliofanywa nchini Marekani yanaonesha kuwa, Waislamu na wafuasi wa dini za waliowachache ni wahanga wa ubaguzi na hisia za chuki nchini humo.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya Pew yenye makao yake makuu Washington, D.C yanaonesha kuwa, asilimia 82 ya wananchi wa Marekani wanaamini kwamba, wafuasi wa dini za waliowachache hususan Waislamu nchini humo wanasumbuliwa na ubaguzi mkubwa.
Taasisi hiyo ya uchunguzi wa maoni imetangaza kuwa, wasiwasi huo umejitokeza nchini Marekani kutokana na propaganda chafu za rais mteule wa nchi hiyo, Donald Trump wakati wa kampeni za uchaguzi.
Ripoti ya Pew inasema kuwa, katika kampeni zake za kabla ya uchaguzi wa Marekani, Trump alitoa madai ya uongo dhidi ya Waislamu na kuchochea hasira na dhana mbaya za watu wa Marekani dhidi ya Waislamu.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na Pew pia yanaonesha kuwa, ubaguzi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika umeongezeka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kutoka asilimia 22 hadi 41.
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais, Donald Trump alitoa wito wa kutumiwa mbinu za kipindi cha dikteta wa zamani wa Ujerumani, Adolph Hitler, kwa ajili eti ya kuwadhibiti Waislamu. Vilevile ametoa wito wa kuzuiwa Waislamu kuingia nchini Marekani.