UN: Wajiri elfu tano wamekufa maji wakieleka Ulaya mwaka huu 2016
Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) limesema wakimbizi na wahajiri wapatao 5,000 wamepoteza maisha mwaka huu wa 2016 wakijaribu kuingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea.
Joel Millman, msemaji wa shirika hilo amesema idadi hiyo imeongezeka baada ya watu 100 kufa maji Alkhamisi iliyopita, baada ya boti mbili walizokuwa wakisafiria kuzama katika Lango la Sicily, katikati ya Italia na Libya.
Naye William Spindler, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR amesema kiwango hicho cha vifo baharini cha mwaka huu kimevunja rekodi na kwamba hakuna mwaka ambao umewahi kushuhudia vifo vya wahajiri baharini kiasi hiki.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Shirika la Uhajiri Duniani, tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2016 hadi sasa, zaidi ya wahajiri laki tatu na nusu wameingia barani Ulaya kwa njia ya baharini.
Mwaka 2015 karibu wakimbizi milioni moja waliingia Ulaya kupitia Bahari ya Mediterranea huku wengine 3,700 wakipoteza maisha au kutoweka katika safari hiyo hatari. Shirika la Kimataifa la Wahajiri limetangaza kuwa Libya ndio njia kuu inayotumiwa na wahajiri wengi licha ya nchi hiyo kukabiliwa na mgogoro wa ndani.
Mwezi Novemba mwaka huu, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilianzisha uchunguzi juu ya biashara haramu ya kuwasafirisha wahajiri wa Kiafrika wanaopelekwa barani Ulaya kupitia usafiri hatari wa baharini.
Fatou Bensouda, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC aliliambia shirika la habari la AFP kuwa, mahakama hiyo imeanzisha uchunguzi ili kubaini iwapo magendo ya wahajiri hao wa Kiafrika wanaopelekwa barani Ulaya, yana uzito sawa na jinai za kivita au la.