Putin ampongeza Bashar Assad kwa kukombolewa kikamilifu Aleppo
Rais Vladimir Putin wa Russia amempigia simu mwenzake wa Syria, Bashar al-Assad, na kumpongeza kutokana na kukombolewa kikamilifu mji wa Aleppo (Halab), uliokuwa ukishikiliwa na magaidi huko kaskazini mwa Syria.
Taarifa ya Ikulu ya Russia (Kremlin) imesema kuwa, Rais Putin amewasiliana na Rais Assad wa Syria kwa njia ya simu na kumpongeza kutokana na kukamilika operesheni ya kuukomboa mji huo wa kistratajia.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Ushindi huo umepatikana kutokana na juhudi za pamoja za kuutokomeza ugaidi wa kimataifa uliotwishwa Syria."
Putin amemwabia Assad kuwa, kilichobakia sasa ni kufanya juu chini kuona mgogoro wote unaoikabili Syria unapatiwa ufumbuzi mara moja.
Siku ya Alkhamisi, Rais Bashar al-Assad wa Syria alisema kukombolewa kikamilifu mji wa kistratejia wa Aleppo (Halab), kaskazini magharibi mwa nchi ni ushindi mkubwa sio tu kwa taifa hilo, bali pia kwa Iran na Russia.
Usiku wa kuamkia jana Ijumaa, wakazi wa mji huo walitoka mabarabarani kwa shangwe, vifijo na vigelegele, baada ya kupokea habari za kukombolewa kikamilifu mji huo, uliokuwa moja ya ngome kuu za wanachama wa magenge ya kigaidi nchini Syria.