Moscow: Ndege ya Russia haikuangushwa na magaidi
Mkuu wa Kamati ya Ulinzi nchini Russia amepinga uwezekano kuwa magaidi walihusika katika kuanguka ndege ya nchi hiyo mapema hii leo.
Ndege hiyo ya kijeshi yenye nambari ya usajili Tu-154 iliyokuwa imebeba abiria 83 na wahudumu tisa imeanguka mapema leo Jumapili katika anga ya Russia katika Bahari Nyeusi muda mfupi baada ya kutoweka kwenye rada.
Victor Ozerov, Mkuu wa Kamati ya Ulinzi Russia amesema kuna uwezekano mkubwa ndege hiyo imeanguka kutokana na sababu za kiufundi au kosa la mwanadamu.
Rais Vladimi Putin wa Russia ametaka kufanyike uchunguzi wa kina kuhusu sababu ya kuanguka ndege hiyo.
Habari zaidi zinasema kuwa, ndege hiyo ilikuwa imebeba wanajeshi, waandishi wa habari na wasanii, wakielekea katika mkoa wa Latakia nchini Syria.
Russia ambayo ina vituo viwili vya jeshi la anga nchini Syria, imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya magaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu, kutokana na ombi la serikali ya Damascus.