Jan 01, 2017 04:38 UTC
  • 70 wauawa, kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi Instabul, Uturuki

Makumi ya watu wanaripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi iliyofanyika usiku wa kuamkia leo katika klabu moja ya anasa mjini Instabul nchini Uturuki.

Vasip Sahin, Gavana wa Istanbul amewaambia waandishi wa habari kuwa, mtu aliyekuwa amevalia nguo za Baba Krismasi (Santa Clause) alimuua afisa wa polisi kabla ya kuingia katika klabu hiyo ambapo mamia ya watu walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya kuukaribisha mwaka mpya wa Miladia wa 2017 na kisha akaanza kuwafyatua risasi ovyo ambapo ameua na kuwajeruhi wengi.

Anbulensi ikiwabeba majeruhi wa hujuma ya kigaidi Istabul

Gavana huyo wa Instabul amesema kwa akali watu 35 wamethibitishwa kufariki dunia katika hujuma hiyo huku wengine zaidi ya 40 wakiachwa na majeraha ya risasi. Imearifiwa kuwa klabu hiyo ilikuwa na watu kati ya 500 na 600 wakati wa hujuma hiyo ya jana usiku inayoaminika kuwa ya kigaidi.

Haya yanajiri wiki tatu baada ya mashambulizi pacha ya kigaidi kutekelezwa karibu na uwanja wa mpira wa Istanbul na kusababisha vifo vya watu 44 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 155. Aidha mwezi Juni mwaka uliomalizika, watu karibu 300 waliuawa na kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi dhidi ya uwanja wa ndege wa Ataturk nchini Uturuki.

Wapiganaji wa PKK

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh na kundi la PKK yamekuwa yakituhumiwa kuhusika na wimbi la mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyoitikisa Uturuki kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa.

Tags