Jamii ya kimataifa yapongeza msimamo wa Senegal dhidi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i22747-jamii_ya_kimataifa_yapongeza_msimamo_wa_senegal_dhidi_ya_israel
Jamii ya kimataifa imeipongeza Senegal kwa kuunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 03, 2017 10:16 UTC
  • Jamii ya kimataifa yapongeza msimamo wa Senegal dhidi ya Israel

Jamii ya kimataifa imeipongeza Senegal kwa kuunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Hii ni licha ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwaita nyumbani wanadiplomasia wake kutoka Senegal sambamba na kutangaza kuikatia nchi hiyo ya Kiafrika misaada na ufadhili. Aidha Waziri Mkuu wa utawala huo bandia Benjami Netanyahu katika hatua ya kutoa jibu dhidi ya msimamo huo wa Senegal katika Baraza la Usalama, amefuta safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika huko Israel iliyotazamiwa kufanyika hivi karibuni.

Hata hivyo, Seydou Gueye, msemaji wa serikali ya Senegal amesema hawajapokea ujumbe wowote kutoka Israel kuhusu hatua hizo za Israel na haswa kukatiwa misaada na kusisitiza kuwa, nchi hiyo itatoa radiamali yake itakapopokea taarifa rasmi kutoka Tel Aviv.

Ramani ya Senegal

Amesema jamii ya kimataifa na hususan nchi za Kiislamu zimeeleza kufurahishwa kwao na msimamo huo wa Senegal katika Baraza la Usalama kuhusu kadhia ya Palestina na kubainisha kuwa, nchi hiyo tangu mwaka 1975, imekuwa mwanachama wa Kamati ya Kutetea Haki za Wapalestina ya Umoja wa Mataifa.

Itakumbukwa kuwa, katika hatua isiyo ya kawaida, Disemba 23 mwaka uliomaizika, Baraza la Usalama la UN lilipasisha azimio hilo kutokana na muswada uliopendekezwa na nchi nne za Malaysia, Venezuela, Senegal na New Zealand likilaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina na kutaka ukomeshwe.

Vitongoji haramu vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina

Azimio hilo lilipasishwa na nchi 14 wanachama wa Baraza la Usalama mkabala wa kura moja tu ya Marekani ambayo ilikataa kulipigia kura.