Waafghani waandamana dhidi ya Pakistan kwa kuhusika katika miripuko
Mamia ya raia wa Afghanistan wamefanya maandamano mjini Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo wakiilaumu Pakistan kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi yao.
Habari kutoka Kabul zimeripoti kwamba, waandamanaji hao wamepiga kambi mbele ya ubalozi wa Pakistan mjini Kabul, wakilalamikia hatua ya jeshi na shirika la upelelezi la nchi hiyo ya kuingilia masuala ya ndani ya Afghanistan na kuratibu miripuko ya mabomu iliyotokea hivi karibuni katika maeneo tofauti ya nchi hiyo.
Waandamanaji hao wametoa nara dhidi ya serikali ya Islamabad na wameitaka serikali ya Kabul kufunga haraka ubalozi wa Pakistan nchini humo. Aidha washiriki katika maandamano hayo wameitaka jamii ya kimataifa kuishinikiza Pakistan ili ihitimishe uungaji mkono wake kwa wanachama wa kundi la kigaidi la Taleban sanjari na kulitambua genge hilo kuwa ni la kigaidi.
Wiki iliyopita miji kadhaa ya Afghanistan ukiwemo mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul, Helmand na Qandahar ilikumbwa na miripuko kadhaa ambapo mamia ya watu waliuawa na wengine kujeruhiwa. Kundi la Taleban limetangaza kuwa limehusika na hujuma hizo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumamosi ya leo serikali ya Afghanistan imetangaza kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kudhibiti asilimia 65 ya ardhi yote ya nchi hiyo kutoka kwa wanachama wa Taleban na al-Qaidah.