Mpambano wa mapema baina ya Trump na vyombo vya habari
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24105-mpambano_wa_mapema_baina_ya_trump_na_vyombo_vya_habari
Rais mpya wa Marekani na timu yake wameanza vita na mpambano na vyombo vya habari katika siku hizi za mwanzoni kabisa mwa kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jan 23, 2017 04:41 UTC
  • Mpambano wa mapema baina ya Trump na vyombo vya habari

Rais mpya wa Marekani na timu yake wameanza vita na mpambano na vyombo vya habari katika siku hizi za mwanzoni kabisa mwa kushika hatamu za uongozi wa nchi hiyo.

Gazeti la Le Monde la Ufaransa limeandika kuwa, Rais mpya wa Marekani, Donald Trump na timu ya baraza lake la mawaziri wamekabiliana uso kwa uso na vyombo vya habari siku mbili tu baada ya kiongozi huyo kuingia Ikulu ya White House na wametambua mapema kwamba, vyombo vya habari ni adui wao.

Msemaji wa White House, Sean Spicer ameyakosoa vikali magazeti na vyombo vya habari kutokana na kukadiria idadi ya watu walioshiriki katika sherehe za kuapishwa Donald Trump. Lililowagusa zaidi wanachama wa timu ya Trump ni zoezi la vyombo vya habari kulinganisha na kupimanisha idadi ya watu walioshiriki katika sherehe hizo na wale walioshiriki katika sherehe za kuapishwa rais aliyemaliza muda wake wa Marekani, Barack Obama.

Mshauri wa Rais Donald Trump, Kellyanne Conway pia jana Jumapili alizusha tena mjadala wa zoezi la vyombo vya habari kukadiria idadi ya watu walioshiriki kwenye sherehe za kuapishwa rais mpya wa nchi hiyo na kusema vyombo vya habari vinasema uongo.

Image Caption

Kimsingi maafisa wa White House huwa hawazungumzii tathmini na makadirio ya idadi ya watu katika matukio mbalimbali na njia pekee ya kukadiria kiwango cha watu walioshiriki katika sherehe za kuapishwa Donald Trump ni uchunguzi wa picha zilizochukuliwa kutokea angani na kufanya ulinganisho na zile za sherehe ya kupishwa Barack Obama hapo mwaka 2009.

Msemaji mwanagenzi wa White House anadai kwamba, picha za sherehe ya kuapishwa Trump zimechukuliwa kwa njia ambayo inaonesha idadi ya watu waliohudhuria sherehe hiyo kuwa ni wachache kuliko wale walioshiriki sherehe ya kuapishwa Obama. Hata hivyo Sean Spicer hakuashiria hata kidogo idadi kubwa ya Wamarekani wanaokadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja walioshiriki katika maandamano na kupinga urais wa Donald Trump katika miji na maeneo mbalimbali ya Marekani siku moja tu baada ya kuapishwa. Alisema anamuachia Trump mwenyewe jukumu la kuzungumzia kadhia hiyo!

Image Caption

Wakati na baada ya kuapishwa Donald Trump Ijumaa iliyopita maelfu ya wananchi wa Marekani walimiminika mjini Washington na katika miji mingine ya nchi hiyo kupaza sauti zao wakieleza hasira na wasiwasi wao kuhusu urais wa Donald Trump. Maandamano hayo pia yaliwashirikisha wanasiasa na watu mashuhuri wa Marekani. Vilevile sherehe za kuapishwa Trump kuwa rais wa 45 wa Marekani zilisusiwa na wabunge na wanasiasa mashuhuri wa Marekani wakionesha upinzani wao dhidi ya siasa zilizotangazwa na kiongozi huyo.

Bustan ya National Mall, Washington DC

Siku hiyo vyombo mbalimbali duniani vilionesha picha za kuapishwa Donald Trump na kufanya ulinganisho baina ya picha hizo na zile za mwaka 2009 wakati Barack Obama alipoapishwa. Ulinganisho huo umeonesha kuwa, idadi ya watu walioshiriki sherehe za kuapisha Obama ni kubwa zaidi kuliko wale waliooneka Ijumaa iliyopita wakati wa kuapishwa Trump. Picha hizo zilionesha kuwa, baadhi ya maeneo ya Bustani ya National Mall mjini Washngton DC yalikuwa wazi bila ya watu na kwamba idadi ya wale walioshiriki sherehe za kuapishwa Obama ilikuwa kubwa zaidi. Suala hilo halikuwafurahisha wanachama wa timu ya Trump ambao wameamua kuvivalia glovu vyombo vya habari na kuvituhumu kuwa vinasema uongo.