Hijabu ya Kiislamu yapigwa marufuku maeneo ya umma Austria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i24531-hijabu_ya_kiislamu_yapigwa_marufuku_maeneo_ya_umma_austria
Serikali ya Austria imechukua hatua ya kuwapiga marufuku wanawake Waislamu kuvaa aina ya hijabu inayofunuka uso wote, yaani niqabu, katika maeneo yote ya umma nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2017 00:51 UTC
  • Hijabu ya Kiislamu yapigwa marufuku maeneo ya umma Austria

Serikali ya Austria imechukua hatua ya kuwapiga marufuku wanawake Waislamu kuvaa aina ya hijabu inayofunuka uso wote, yaani niqabu, katika maeneo yote ya umma nchini humo.

Chama tawala cha Austria kimedai kimechukua hatua hiyo kwa kuhofia kuwa chama chenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia cha Freedom Party kitatumia suala la uvaaji niqabu kuibua hisia dhidi ya wageni na kuingia madarakani kwa wimbi hilo.

Kansela Christian Kerr  wa Austria,ambaye anaongoza muungano tawala  wa vyama vya SPO na OVP, amesema marufuku ya vazi linalofunika uso kikamilifu katika sehemu za umma itatekelezwa hatua kwa hatua katika kipindi cha miezi 18 ijayo. 

Katika miezi ya hivi karibuni, chama hicho cha Freedom Party kinaonekana kuongoza katika uchunguzi wa maoni ikiwa ni muendelezo wa vyama vya kibaguzi kupata umashuhuri Ulaya hasa baada ya ushindi wa Donald Trump kama rais wa Marekani.

Mwanamke Mwislamu akiwa amevaa niqabu katika eneo la umma

Bunge la Ufaransa pia nalo miezi sita iliyopita lilipitisha sheria sawa na hiyo ya Austria ya kupiga marufuku nikabu katika maeneo ya umma. Ubelgiji, na baadhi ya maeneo ya Uholanzi nayo pia yamepiga marufuki vazi hilo.

Naye Kansela Angela Merkel wa Ujerumani pia mwezi uliopita katika kikao cha chama chake cha Wademokrat Wakristo alisema niqabu inayovaliwa na wanawake Waislamu inapaswa kupigwa marufuku katika maeneo ya umma.