Madai ya Trump kuhusu kuanza sera mpya za kigeni za Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani, akizungumza katika sherehe za kuapishwa Rex W. Tillerson kama waziri mpya wa mambo ya nje wa nchi hiyo, amesema wakati umefika kwa sera za kigeni kusimamiwa na mtu mwenye macho ya wazi ili aweze kuutazama ulimwengu kwa macho mapya kwa lengo la usuluhishaji wenye kuzingatia ukweli wa kale.
Trump aidha amesema serikali yake imerithi changamoto kubwa Mashariki ya Kati na dunia lakini pamoja na hayo kunaweza kupatikane amani na usalama duniani.
Trump amesisitiza kuhusu uwezo wa waziri mpya wa mambo ya nje na kusema katika sera zake za kigeni, Marekani inahitaji dunia yenye amani na usalama. Kauli ya Trump kuwa Marekani inahitaji usalama na amani duniani imetolewa wakati ambao katika wiki ya kwanza ya utawala wake, aliwapiga marufuku watu milioni 150 kutoka nchi saba za Kiislamu kuingia katika ardhi ya Marekani. Hali kadhalika Trump amemteua jenerali mstaafu Michael Flynn kuwa mshauri wake wa usalama wa taifa punde baada ya kuapishwa Tillerson. Katika kauli yake ya awali, Flynn ametoa matamshi yaliyojaa uhasama na kusema Marekani itakabiliana na mpango halali wa makombora ya kujihami ya Iran.
Katika kipindi cha siku 10 za kwanza za utawala wa Donald Trump, kumeshuhudiwa matamshi yenye utata, yaliyojaa uhasama na yenye kuvuruga uthabiti wa Asia Magharibi (Mshariki ya Kati) maingiliano na Ulaya, ushirikiano na China na kuanzishwa mfumo mpya wa makombora.
Katika kipindi chake cha kampeni za uchaguzi, Trump alikosoa mara kadhaa uingiliaji wa Marekani katika masuala ya dunia.
Kwa mfano, alikosoa wazi serikali ya Warepublican ya George W Bush na pia serikali ya Obama kwa kutumia dola trilioni sita katika vita Asia Magharibi baada ya matukio ya Septemba 11 na kusema vita hivyo havikuwa kwa manufaa ya Marekani.
Matamshi hayo ya Trump yalipelekea apate uungaji mkono wa umma wa Marekani na hivyo kupelekea apate ushindi katika uchaguzi wa rais.
Pamoja na hayo, hivi sasa baada ya kukalia kiti cha urais, Trump hajaonyesha azma yoyote ya kubadlisha mkondo wa muda mrefu wa seria za kigeni na sera za kiusalama za Marekani.
Hata tunaweza kusema kuwa, hivi sasa viongozi wa Marekani wanaonyesha kiburi kikubwa zaidi na kujihisi kuwa bora duniani. Hii ni hisia iliyoibuka miaka 70 iliyopita baada ya kumalizika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Nara kama vile, "Nataijenga Marekani Yenye Nguvu Tena", "Marekani Itangulizwe" au "Nunua Bidhaa za Marekani na Waajiri Wamarekani" ingawa zilionyesha kuwa Trump ataelekeza sera zake katika masuala ya ndani ya nchi lakini pia ni nara zinazoashiria namna Washignton inavyofuatilia sera za ubinafsi na kutoshirikiana na madola mengine katika uga wa kimataifa.
Sawa na marais wengine wa Marekani ambao katika zama za kampeni hutoa ahadi za kuwahadaa wananchi, Trump pia alitoa ahadi za kufanyika mabadiliko ya kimsingi katika sera za kigeni na za ndani ya Marekani. Lakini uzoefu unaonyesha kuwa, marais wa Marekani baada ya muda husahau ahadi zao za uchaguzi au huzibadilisha kutokana na upinzani wa kisiasa.
Kwa hivyo, madai ya Trump kuwa Marekani inahitaji amani au sisitizo la kubadilisha mtazamo kuhusu dunia, tena wiki mbili tu baada ya kuanza serikali mpya, ni jambo lisiloweza kuashiria kuwepo mabadiliko katika sera za kigeni za Marekani.