CIA yaipa Saudia tuzo ya "kupambana na ugaidi"
Shirika Kuu la Kijasusi Marekani (CIA) limempa tuzo Mrithi wa Kiti cha Ufalme Saudi Arabia, Mohammad bin Nayef kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni "kazi zake za kijasusi katika vita dhidi ya ugaidi."
Mkuu wa CIA, Micheal Pompeo alimkabidhi Nayef 'Nishani ya George Tenet' katika sherehe zilizofanyika mjini Riyadh, Saudi Arabia siku ya Ijumaa.
Walioshiriki katika sherehe hizo ni Naibu wa Mritihi wa Kiti cha Ufalme Muhammad Bin Salman ambaye pia ni waziri wa ulinzi pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu wa Saudi Arabia.
Katika sherehe hizo, Nayef alidai Saudia inaongoza vita dhidi ya ugaidi na kusema eti ufalme huo unapinga aidiolojia zote za kidini, kisiasa na kijamii zinazoeneza ugaidi.
Madai hayo yanatolewa wakati ambapo, Saudi Arabia ndio chimbuko la pote la Uwahhabi ambalo linaeneza na kutekeleza vitendo vya kigaidi. Makundi makubwa zaidi ya kigaidi duniani ni ya Kiwahhabi na hupokea misaada ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kutoka kwa utawala wa Saudi Arabia. Kati ya makundi hayo ni ISIS au Daesh, Al Qaeda, Al Shabab, Boko Haram, Taliban n.k. Makundi hayo huwakufurisha Waislamu wasiofuata itikadi zao potofu.
Afisa huyo wa Saudia amepokea medali hiyo ya kupambana na ugaidi katika hali ambayo kwa muda wa takriban miaka miwili sasa Saudia imekuwa ikidondosha mabomu katika nchi jirani na maskini ya Yemen na hadi hivi sasa imeshapelekea karibu watu 12,000 kupoteza maisha wengi wakiwa ni raia hasa wanawake na watoto wadogo.