Palestina yaendelea kutambuliwa kimataifa, Marekani yashindwa kuitetea Israel
Pamoja na kuwa Marekani inaendelea kuunga mkono kikamilifu utawala wa Kizayuni wa Israel, gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth limeandika kuwa, balozi za Palestina zinaendelea kuongezeka duniani na hata kuzishinda zile za Israel.
Gazeti hilo limeandika kuwa hivi sasa kuna ofisi 103 za uwakilishi wa kidiplomasia huko Palestina ikilinganishwa na 102 zilizoko Tel Aviv. Aidha gazeti hilo limeandika kuwa katika hali ambayo Palestina ina ofisi 95 za uwakilishi wa kidiplomasia katika maeneo mbali mbali duniani, utawala wa Israel una ofisi 78 pekee za uwakilishi duniani.
Gazeti la Kizyauni la Yedioth Ahronoth limekiri ukweli huu na kuongeza kuwa hivi sasa mikakati ya kuitambua rasmi Palestina katika nchi zote za dunia imeshika kasi na jambo hili linathibitisha wazi kuwa aghalabu ya nchi duniani zinautazama utawala wa Kizayuni wa Israel kama utawala bandia.
Mwaka 2012 Palestina ilitambuliwa kama mwanachama mtazamaji wa Umoja wa Mataifa na mwaka huo huo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likawasilisha mpango wa kutambuliwa rasmi Palestina kama nchi.
Ingawa hivi sasa Palestina ina ofisi 95 za uwakilishi wa kidiplomasia kote duniani, lakini kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina, hadi sasa kuna nchi 135 duniani ambazo zimeitambua Palestina kama nchi huru.

Kwa hivyo, Palestina ikipata uwezo itatuma wawakilishi katika nchi zote hizo 135. Si tu kuwa Palestina inaendelea kutambuliwa na nchi tofauti duniani bali hata shakhsia mbali mbali wa Palestina wanaandaliwa kuchukua majukumu muhimu ya kimataifa.
Ni kwa msingi huo ndio Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akamteua Salam Fayadh Waziri Mkuu wa Zamani wa Palestina na mmoja kati ya viongozi wa kisiasa wa Harakati ya Fat'h kuwa mwakilishi wake katika mazungumzo ya amani nchini Libya.
Lakini punde baada ya uteuzi huo, serikali mpya ya Marekani ambayo ni mtetezi sugu wa Israel imepinga kuteuliwa Mpalestina huyo. Serikali ya Donald Trump imepinga uteuzi huo ili kuulinda utawala wa Kizayuni ambao itibari yake inazidi kuporomoka kimataifa. Nikki Haley mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa amezungumza katika Baraza la Usalama na kuutetea utawala wa Kizayuni wa Israel. Amedai kuwa Umoja wa Mataifa umekuwa ukichukua maamuzi kwa maslahi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na kwa madhara ya Marekani na Israel. Aidha amesema katika siku za usoni, Marekani haitaunga mkono Israel kwa maeneno tu bali itachukua hatua za kivitendo.
Tukiangazia hatua ya nchi nyingi kutambua rasmi Palstina tunafikia natija kuwa nchi hizo kwa njia isiyo ya moja kwa moja zinalaani jinai za utawala haramu wa Israel.
Hatua ya Marekani kupinga kuteuliwa Salam Fayadh kama mwakilishi mpya wa Umoja wa Mataifa Libya ni jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa, iwapo Marekani ingesitisha mashinikizo yake kwa nchi mbali mbali na pia kuacha kuiunga mkono Israel, basi leo tungeshuhudia nchi zote duniani na taasisi zote za kimatiafa zikichukua hatua imara na za kivitendo katika kulaani jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.