Amnesty International yatahadharisha kuhusu kushtadi ukandamizaji Bahrain
https://parstoday.ir/sw/news/world-i25168-amnesty_international_yatahadharisha_kuhusu_kushtadi_ukandamizaji_bahrain
Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limetahadharisha kuhusu kuendelea kukandamizwa kwa kiasi kikubwa raia huko Bahrain kunakofanywa na utawala wa Aal Khalifa.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Feb 15, 2017 04:26 UTC
  • Amnesty International yatahadharisha kuhusu kushtadi ukandamizaji Bahrain

Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limetahadharisha kuhusu kuendelea kukandamizwa kwa kiasi kikubwa raia huko Bahrain kunakofanywa na utawala wa Aal Khalifa.

Amnesty International imetangaza kuwa mgogoro wa haki za binadamu ni mkubwa sana huko Bahrain na kwamba ukandamizaji uliongezeka katika wiki kadhaa zilizopita nchini humo; huku wananchi wakiendelea kukandamizwa, kunyongwa na kutiwa mbaroni kiholela. 

Katika taarifa yake Shirika la Amnesty International limewataka watawala wa Bahrain kujiepusha kuamiliana na waandamanaji kwa mabavu sambamba na maadhimisho ya mwaka wa sita wa vuguvugu la mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Bahrain. Taarifa ya Amnesty International imesisitiza kuwa, hali ya Bahrain imekuwa ya mgogoro na kwamba katika kipindi cha miezi miwili ya mwanzo wa mwaka huu, kumeshuhudiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa vitendo vya mabavu na utumiaji nguvu kiholela na vya uchupaji mipaka vinavyofanywa na askari usalama wa utawala wa Bahrain dhidi ya raia wa nchi hiyo. Taarifa ya Shirika la Msamaha Duniani imeongeza kuwa, kunyongwa kiholela raia huko Bahrain kumekuwa kukishuhudiwa nchini humo tangu mwaka 2011. 

Makabiliano kati ya polisi wa utawala wa Aal Khalifa na waandamanaji

Amnesty imesema kuwa, watawala wa Bahrain wanapasa kuheshimu haki,  uhuru wa kujieleza na ule wa raia wa kufanya mikutano na maandamano, na kuacha kuwanyonga watu; la sivyo kuna hatari kubwa ya kutokea mgogoro wa haki za binadamu nchini humo.