Ujerumani yaonya Israel itaibua vita kupora ardhi zaidi za Wapalestina
Ujerumani imeonya kuwa hatua ya utawala haramu wa Israeli ya kunyakua ardhi zaidi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni jambo litakaloibua vita vipya Mashariki ya Kati.
Waziri wa Mambo ya Nje ya Ujerumani Sigmar Gabriel amebaiisha wasiwasi wake kuhusu ongezeko la ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zilizoporwa na Israel. Amesema hatua hiyo itapelekea kutowezekana kupatikana suluhisho la kile kinachotajwa kuwa ni 'nchi mbili' na badala yake kuibua vita.
Kauli ya Gabriel imekuja siku moja baada ya Rais Donald Trump kusema Marekani haitofuatilia tena 'suluhisho la nchi mbili' katika mgogoro wa Palestina na Israel. Sera hiyo mpya ya Marekani imelaaniwa vikali na Wapalestina na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa.
Uhusiano wa Ujerumani na Israel umezorota katika siku za hivi karibuni baada ya wakuu wa Berlin kusema waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu hafungamani tena na kile kinachotajwa kuwa ni mcakato wa amani Mashariki ya Kati hasa 'suluhisho la nchi mbili' yaani Palestina ikubali kuwa nchi katika ardhi ilizonazo hivi sasa na Israel iendelee kukalia ardhi ilizonyakua za Wapalestina.
Harakati za mapambano ya Kiislamu Palestina zinapinga suluhisho hilo na zinataka utawala bandia wa Israel uondoke kikamilifu katika ramani ya Palestina.