Umoja wa Mataifa walaani shambulizi la kigaidi nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i25390-umoja_wa_mataifa_walaani_shambulizi_la_kigaidi_nchini_somalia
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Somalia, amelaani shambulizi la kigaidi katika soko moja la Mogadishu, mji mkuu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2017 04:34 UTC
  • Umoja wa Mataifa walaani shambulizi la kigaidi nchini Somalia

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Somalia, amelaani shambulizi la kigaidi katika soko moja la Mogadishu, mji mkuu wa nchi hiyo.

Michael Keating, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia mbali na kulaani mlipuko wa bomu uliotokea jana katika soko amesema kuwa, kuwaua raia wasio na hatia ni kitendo cha kuchukiza sana.

Michael Keating, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia

Keating ameongeza kuwa wahusika wa shambulizi hilo wanatakiwa kufikishwa haraka mbele ya vyombo vya sheria. Shambulizi la Jumapili ya jana katika soko mjini Mogadishu lilipelekea kwa akali watu 30 kuuawa na zaidi ya 40 kujeruhiwa. Wengi wa wahanga wa hujuma hiyo ya kigaidi walikuwa ni wapita njia na wauzaji wa bidhaa za maduka ambao walikuwa sokoni wakati wa kujiri shambulizi hilo. Shambulizi hilo lilitokea katika hali ambayo Somalia inajiandaa kushuhudia kuapishwa rais mpya wa nchi hiyo, Mohamed Abdullahi Mohamed Farmajo. Hii sio mara ya kwanza kwa vituo vya kibiashara nchini Somalia kushambuliwa na makundi ya wabeba silaha wasiojulikana.

Wanachama wa kundi la kigaidi la ash-Shabab nchini Somalia

Mara nyingi hujuma hizo zimekuwa zikitekelezwa na wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah. Hivi karibuni pia kundi hilo lilitangaza kuhusika na hujuma dhidi ya askari usalama wa Somalia na wale wa Umoja wa Afrika AMISOM.