Jumuiya za Kiislamu Marekani zaonya kuhusu kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu
Baraza la Mahusiano ya Uislamu na Marekani (CAIR) limetahadharisha kuhusiana na kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.
Mmoja wa viongozi wa Baraza la Mahusiano ya Uislamu na Marekani amesema, viongozi wa Marekani wamenyamazia kimya suala la kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu pamoja na hujuma zinazofanywa dhidi ya misikiti.
Viongozi wa Baraza la Mahusiano ya Uislamu na Marekani CAIR wamesisitiza kuwa, ubaguzi dhidi ya Waislamu umeongezeka nchini humo na kwamba, Rais Donald Trump wa nchi hiyo hapaswi kunyamazia kimya suala hilo.
Inaelezwa kuwa, tangu Rais Donald Trump wa Marekani achukue hatamu za uongozi, mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu umeongezeka nchini humo na kwamba, baadhi ya misikiti imebomolewa na wakati mwingine imekuwa ikichomwa moto.
Wanachuo wa Kiislamu wa Vyuo Vikuu nchini Marekani wamekuwa wakihujumiwa na kushambuliwa kutokana na kukithiri propaganda chafu na matangazo ya kibaguzi.
Licha ya kuongezeka propaganda chafu dhidi ya Uislamu lakini idadi ya watu wanaosilimu na kuingia katika dini hii tukufu imekuwa ikiongezeka kwa kasi mno katika ulimwengu wa Magharibi.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa, Uislamu ndiyo dini inayokuwa kwa kasi zaidi katika ulimwengu wa Magharibi.