Trump asema Obama anaongoza maandamano, uvujaji siri
Rais Donald Trump wa Marekani amesema mtangulizi wake, Barack Obama, ndiye binafsi anayesimamia uvujishaji wa sira za serikali na maandamano dhidi yake yanayoendelea kote katika nchi hiyo.
Katika mahojiano na Televisheni ya Fox News ambayo yamerushwa hewani leo Jumanne, Trump alipoulizwa iwapo anadhani watu katika utawala ulioondoka wa Obama wanahusika na maandamano na hatua zingine dhidi yake, alisema Obama binafsi anahusika na njama hizo. Pasina kutoa ushahidi, Trump alisema hakuna shaka kuwa Obama anaongoza maandamano na uvujaji wa siri za serikali.

Maafisa kadhaa waliokuwa katika kampeni za Obama miaka ya nyuma wamekuwa miongoni mwa wanaoongoza maandamano dhidi ya Trump ambayo yamekuwa yakiendelea tangu aapishwe Januari 20. Aidha Trump amelaumu mashirika ya kijasusi ya FBI na NSA kuwa yalihusika na uvujaji wa siri ambazo zilimlazimu mshauri wake wa usalama wa taifa, jenerali mstaafu Mike Flynn kujiuzulu kutokana na uhusiano wake na Russia.
Katika kukabiliana na wimbi kubwa la maandamano, hivi karibuni maafisa wa sheria wa Marekani walionya kuwa, wanaoandamana dhidi ya Trump watafungwa miaka 10 jela kwa madai ya kufanya machafuko na uasi nchini humo au kulipa faini nzito.