Bunge la Uswisi lapinga muswada wa kupiga marufuku vazi la burqa
Bunge la Uswisi limekataa kupasisha muswada wa kupiga marufuku nchini humo vazi la stara la burqa linalovaliwa na baadhi ya wanawake wa Kiislamu.
Bunge la Juu la Uswisi linalofahamika kama The Council of State limekataa kuunga mkono muswada huo ambao tayari ulikua umepata baraka kamili za Bunge la Chini mwezi Septemba mwaka jana 2016.
Muswada huo wa kupiga marufuku uvaaji wa burqa nchini humo uliandaliwa na wabunge wa chama cha mrengo wa kulia cha Swiss People’s Party, na iwapo ungepasishwa na Bunge la Juu, wanawake wa Kiislamu nchini humo wasingeruhusiwa kuvaa vazi hilo la staha katika maneo ya umma.
Andrea Caroni, mmoja wa wabunge walioupinga muswada huo amesema kupigwa marufuku vazi la burqa nchini humo mbali na kuwa sio jambo la mantiki, lakini pia ni ukiukaji wa uhuru wa kuabudu haswa ikizingatiwa kuwa, asilimia 5 ya wananchi wa Uswisi (milioni 8.2) ni Waislamu.
Nchi kadhaa za magharibi kama vile Bulgaria, Canada, Ubelgiji na Ufaransa zimepiga marufuku vazi hilo la staha, huku Kansela wa Ujerumani Angela Merkel Disemba mwaka jana akitoa wito wa kupigwa marufuku vazi la stara la burqa au niqabu nchini humo, akisisitiza kuwa, sheria ya Ujerumani iko juu ya kanuni na sheria za kidini.
Kadhalika mapema mwaka huu, serikali ya Morocco ilipiga marufuku uzalishaji na uuzaji wa vazi la burqa nchini humo, kutokana na kile kilichotajwa kuwa sababu za kiusalama.