US$ Milioni 255 zahitajika kuwasaidia watoto kukabiliana na njaa Afrika, Yemen
(last modified Thu, 30 Mar 2017 06:42:22 GMT )
Mar 30, 2017 06:42 UTC
  • US$ Milioni 255 zahitajika kuwasaidia watoto kukabiliana na njaa Afrika, Yemen

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limesema, watoto takriban milioni 1.4 nchini Nigeria, Somalia, Sudan Kusini na Yemen wako katika hatari ya kukabiliwa na njaa.

Katika taarifa, UNICEF imetoa wito kwa jamii ya kimataifa ichangie dola za kimarekani milioni 255 ili kukabiliana na hali hiyo..

UNICEF aidha imetahadharisha kuwa hatari ya njaa si kama iko tu katika nchi hizo nne.

Shirika hilo limesema kutokana na machafuko, njaa na ukosefu wa maji, watu wanalazimika kukimbia makazi na kukimbia nchi, na kiwango cha utapiamlo pia kitaendelea kuongezeka katika nchi jirani.

Watoto wengi wanahitaji misaada ya chakula Afrika Mashariki na Magharibi

UNICEF pia imesema watoto waliokimbia makazi hawana huduma za afya na lishe, maji safi, au mazingira safi.

Mwezi Februari Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema baa la njaa limeenea katika nchi kadhaa za Afrika na Yemen huku akisema hali ya Sudan Kusini ni mbaya sana. Alibainisha kuwa watu zaidi ya milioni 20 Sudan Kusini , Somalia, Yemen , na Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wanakabiliwa na njaa na hawana uhakika wa kupata chakula. Alisema kwa mwaka mashirika ya kutoa misaada yanahitaji angalau dola bilioni 4.4 ifikapo mwisho wa Machi ili kuepuka maafa.