Vyama vya mrengo wa kulia Ulaya na tatizo la kuwakubali wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27108-vyama_vya_mrengo_wa_kulia_ulaya_na_tatizo_la_kuwakubali_wakimbizi
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika mkutano na viongozi wa vyama vya mrengo wa kulia barani Ulaya amekiri kuwa bara hilo halijasimamia ipasavyo suala la wakimbizi na wahamiaji.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Mar 31, 2017 10:47 UTC
  • Vyama vya mrengo wa kulia Ulaya na tatizo la kuwakubali wakimbizi

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika mkutano na viongozi wa vyama vya mrengo wa kulia barani Ulaya amekiri kuwa bara hilo halijasimamia ipasavyo suala la wakimbizi na wahamiaji.

Akihutubu mkutano wa 'Vyama vya Watu wa Ulaya' uliofanyika katika mji mkuu wa Malta, Valletta, Merkel amesema wakimbizi na wahajiri wanapaswa kukaribishwa lakini wakati huo huo mipaka ya Ulaya isimamiwe na ilindwe ipasavyo kupitia Polisi ya Ulaya maarufu kama Europol.

Matamshi hayo yametolewa wakati ambao baadhi ya serikali za Ulaya ziko chini ya mashinikizo ya vyama vyenye misimamo mikali vya mrengo wa kulia vikitaka kusitisha sera za kuwapokea wakimbizi.

Aidha katika baadhi ya nchi za Ulaya wakimbizi wanakabiliwa na hujuma za watu wabaguzi na wenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia. Vilevile taasisi za kutetea haki za binadamu zimetahadahrisha kuhusu ongezeko kubwa la makundi ya wale wenye chuki dhidi ya raia wa kigeni.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya vyama vya mrengo wa kulia  vimejipata katika njia pande ya kuchagua moja kati ya njia mbili. Njia ya kwanza ni kutekeleza ahadi zao za kuwakaribisha wakimbizi na hilo linaweza kupelekea kushindwa au kupungua kura zao katika uchaguzi. Njia ya pili ni kufuata wimbi lilioibuliwa na vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo mikali la kupinga wakimbizi na wahajiri barani humo.

Katika uchaguzi wa bunge wiki mbili zilizopita huko Uholanzi, baadhi ya wanasiasa wenye misimamo ya kati ya mrengo wa kulia walionekana kujiunga na sera za vyama vya mrengo wa kulia vyenye misimamo mikali ya kupinga wakimbizi. Mkondo huu unatazamiwa kushuhudiwa katika nchi kadhaa za Ulaya ambazo zitakuwa na chaguzi hivi karibuni hasa Ujerumani na Ufaransa. Kwa msingi huo yamkini sera za Ulaya kuwakubali wakimbizi zikashuhudia mabadiliko makubwa na kupelekea bara hilo kufunga mipaka yake mbele ya wageni na wahajiri.

Kushindwa Umoja wa Ulaya kuchukua msimamo wa wastani katika kuwapokea wahajiri na wale wanaokimbia vita katika nchi zao ni jambo ambalo litakuwa na matokeo mabaya ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama kwa nchi za bara hilo.

Hivi sasa, kutokana na migogoro na ukosefu wa usalama katika nchi za Afrika Kaskazini zinazopakana na Bahari ya Mediteranea hasa Libya, wakimbizi na wahamiaji wengi wanatumia mwanya huo kukimbilia nchi za Ulaya wakitoroka vita na umasikini barani Afrika na nchi za Asia Magharibi au Mashariki ya Kati.

Katika hali kama hii, iwapo bara Ulaya litatekeleza sera za kuwafungia mipaka wakimbizi, nchi zinazopakana na Umoja wa Ulaya na ambazo zinatumiwa kama njia na wakimbizi zitakumbwa na mgogoro wa kibinadamu. Aidha kufungwa kabisa mipaka kutapelekea wafanya magendo ya binadamu kupata soko zaidi la kuwaingiza wakimbizi Ulaya kwa njia za mkato na hatari zaidi ya hivi sasa.

Maandishi ya kupinga wahajiri nja ya kanisa barani Ulaya

Aidha namna ambavyo nchi za Ulaya zinaamiliana na wakimbizi Waislamu ni jambo ambalo limetia doa madai ya bara hilo kuwa mtetezi wa haki za binadamu na kitovu cha  maisha ya maelewano baina ya watu wa itikadi zote. Ni wazi kuwa kutendewa vibaya na kudhulumiwa wakimbizi barani Ulaya, hasa Waislamu, ni jambo ambalo litaibuka hisia za chuki na ulipizaji kisasi miongoni mwa vizazi vya pili na tatu vya wahajiri wa kigeni waliozaliwa Ulaya kutoka nchi za Afrika na Asia Magharibi.

Angela Merkel, kama mmoja kati ya wanasiasa wenye ushawishi katika vyama vya mrengo wa kulia wa wastani barani Ulaya, anajaribu kuzuia wanachama wa vyama hivyo kuhamia katika vyama vya misimamo mikali ya mrengo wa kulia. Pamoja na hayo hakufanikiwa hata ndani ya Ujerumani kwenyewe ambako kunashuhudiwa ongezeko la watu wenye misimamo mikali ya kuwapinga wahajiri.

Ni kwa sababu hii ndio maana Kansela wa Ujerumani hakuweza kufikia malengo yake katika kikao cha viongozi wa vyama vya mrengo wa kulia wa misimamo ya wastani huko Malta.