Kutiliwa nguvu mazungumzo ya Russia na kundi la Taliban la Afghanistan
Alexander Grushko, mwakilishi wa kudumu wa Russia katika shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO amethibitisha habari kuwa Moscow imefanya mazungumzo na kundi la Taliban la Afghanistan.
Amesema, katika mazungumzo yake na kundi hilo, Russia imelenga kulishawishi liheshimu mpango wa umoja wa kitaifa wa Afghanistan kwa mujibu wa misingi iliyoainishwa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amesema, misingi hiyo ni pamoja na kuheshimiwa katiba ya Afghanistan, kuacha mashambulizi ya kutumia silaha pamoja na kukata uhusiano na mtandao wa al Qaida na magenge mengine ya kigaidi. Mwakilishi huyo wa Russia katika shirika la kijeshi la NATO, amekanusha madai yaliyotolewa na kamanda mkuu wa NATO, Jenerali Curtis Scaparrotti aliyedai kuwa Russia inawaunga mkono na kuwapa silaha wapiganaji wa kundi la Taliban. Alexander Grushko amesema, Russia imewatahadharisha viongozi wa NATO wajiepushe na kutoa matamshi yasiyo na mizani.
Matamshi hayo ya mwakilishi wa Russia katika shirika la kijeshi la nchi za Magharibi NATO na kukiri kwamba Moscow imefanya mazungumzo na kundi la Taliban ni hatua zilizochukuliwa katika hali ambayo kuingia Russia kwenye suala la Afghanistan na hatua yake ya kufanya mazungumzo na kundi la Taliban kumesababisha matatizo katika uhusiano wa Kabul na Moscow. Serikali ya Afghanistan imelalamikia vikali jambo hilo.
Hata hivyo Russia inaonekana kufanya juhudi ya kufidia makosa yake kupitia kuitisha kikao cha pande sita mwezi Februari mwaka huu na kuialika pia serikali ya Afghanistan baada ya Kabul kulalamikia vikali mazungumzo ya pande tatu ya mjini Moscow. Hivi sasa Russia imekiri kuwa imefanya mazungumzo na kundi la Taliban na kuhalalisha jambo hilo kwa kusema kuwa mazungumzo hayo hayakutoka nje ya misingi iliyoainishwa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na amani ya Afghanistan.
Hata hivyo inavyoonekana ni kwamba Marekani ndiyo iliyoingia wasiwasi zaidi kuhusu kujiingiza Russia katika mgogoro wa Afghanistan. Marekani haifichi hamaki zake kwa Russia kuhusiana na suala hilo. Ikumbukwe kuwa ni Wamarekani ndio walioungana na mujahidina wa Afghanistan kuwafukuza nchini humo wanajeshi wa Umoja wa Kisovieti katika muongo wa 1980. Inavyoonekana hivi sasa Marekani imejipa hati miliki ya kushughulikia suala la Afghanistan. Ni hivi karibuni tu ambapo Waziri wa Ulinzi wa Marekani alidai kuwa msimamo wa Russia kuhusiana na Afghanistan na kundi la Taliban unaitia wasiwasi Washington. Inaonekana wazi kwamba Marekani imeamua kutumia vibaya wasiwasi ilio nao serikali ya Afghanistan kuhusiana na kutokuwa wazi msimamo wa Russia kuhusu nchi hiyo na pia kuhusiana na kundi la Taliban. Baada ya serikali ya Kabul kuilaumu vikali Russia kwa kufanya mazungumzo na kundi la Taliban, White House nayo imejitokeza na kusema kuwa msimamo wa Moscow kuhusiana na kundi la Taliban na suala zima la Afghanistan unaitia wasiwasi Marekani, ili kwa njia hiyo iweze Washington kuibana Ikulu ya Kremlin na kupunguza kasi ya Russia ya kujiingiza katika mgogoro wa Afghanistan.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, licha ya kwamba serikali ya Afghanistan ina wasiwasi mkubwa kuhusiana na siasa za Russia za kuitisha kikao cha pande tatu cha kuzungumzia suala la Afghanistan huko Moscow bila ya kuishirikisha serikali ya Kabul pamoja na mazungumzo ya siri baina ya Russia na kundi la Taliban, lakini hatua ya Moscow ya kurekebisha makosa ya huko nyuma na kutangaza hadharani kuwa imefanya mazungumzo na kundi la Taliban na lengo la mazungumzo yao, pamoja na hatua ya Moscow ya kuitisha kikao cha pande sita cha amani ya Afghanistan mwezi Februari mwaka huu na kuipa serikali ya Kabul nafasi muhimu kwenye mazungumzo hayo, ni mambo ambayo yanaweza kuondoa wasiwasi ilio nao serikali ya Afghanistan kuhusu msimamo wa Russia juu ya mgogoro wa nchi hiyo.