Kijana Mmarekani akiri kuhusika na njama za kumuua Papa Francis
https://parstoday.ir/sw/news/world-i27288-kijana_mmarekani_akiri_kuhusika_na_njama_za_kumuua_papa_francis
Kijana mmoja Mmarekani kutoka jimbo la New Jersey amekiri mbele ya mahakama kuwa alihusika katika njama zilizofeli za kumuua Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2017 10:46 UTC
  • Kijana Mmarekani akiri kuhusika na njama za kumuua Papa Francis

Kijana mmoja Mmarekani kutoka jimbo la New Jersey amekiri mbele ya mahakama kuwa alihusika katika njama zilizofeli za kumuua Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis.

Inaarifiwa kuwa, Santos Colon mwenye umri wa miaka 17 alishajiishwa kutekeleza ukatili huo kutokana na mapenzi yake kwa kundi la kigaidi la ISIS (Daesh).

Idara ya Mahakama ya Marekani imesema kuwa, kijana huyo amekiri kuwa alikuwa tayari kujiripua sambamba na kukodi mlengaji shabaha stadi (sniper) ili kumuangamiza Papa Francis, wakati alipolitembelea jimbo la Philadelphia, Septemba 27 mwaka 2015.

Hata hivyo njama za barobaro huyo wakati huo akiwa na miaka 15 zilitibuka, baada ya kumpa kibarua hicho bila kujua afisa wa Polisi ya Upelelezi Marekani FBI.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis

Hata hivyo Idara ya Mahakama ya Marekani haijatoa maelezo ni jinsi gani kijana huyo alivutiwa na itikadi na misimamo ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh au iwapo alikuwa na mawasiliano yoyote na kundi hilo au la.

Santos Colon huenda akahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela baada ya kuondolewa mashtaka matatu dhidi yake, na yumkini akaanza kutumikia kifungo hicho mwaka 2021, kwa kuwa timu ya waendesha mashtaka imetaka kijana huyo afanyiwe uchunguzi wa kiakili chini ya ulinzi mkali.