Shambulizi la Marekani lafeli Syria, ndege zaanza kuruka kama kawaida
Siku moja baada ya Marekani kufanya shambulio la makombora dhidi ya uwanja wa ndege wa jeshi la anga la Syria wa Shayrat huko Homs, ndege za kivita za Syria zimeanza kuruka kama kawaida kwa ajili ya kuendeleza mapambano dhidi ya magaidi wanaoungwa mkono na Marekani na vibaraka wake.
Shirika la habari la Reuters limelinukuu kundi linalodaiwa la kutetea haki za binadamu lenye makao yake mjini London Uingereza na ambalo liko karibu na magaidi wa Syria likisema kuwa, ndege za kivita za Syria zimeanza kupaa kutoka katika uwanja wa ndege wa Shayrat baada ya uwanja huo kushambuliwa kwa makombora ya Tomahawk ya Marekani. Ndege za Syria zimefanya mashambulizi dhidi ya magaidi wa Daesh katika viunga vya mji wa Tadmur (Palmyra) mashariki mwa Homs kutokea uwanja huo wa ndege.
Wanaharakati wa Syria wanasema kuwa, hasara zilizosababishwa na shambulio la makombora ya Marekani kwenye uwanja huo wa ndege hazijulikani, lakini inaonekana Marekani imefeli kwenye shambulio lake hilo la kivamizi, kwani ndege za Syria zimeanza kuruka kama kawaida kutoka kwenye uwanja huo.
Ikumbukwe kuwa mapema Ijumaa asubuhi, Marekani ilivurumisha makombora 59 aina ya Tomahawk dhidi ya uwanja wa ndege wa Shayrat wa jeshi la serikali ya Syria huko Homs kwa madai yasiyothibitishwa ya kwamba eti Syria imefanya mashambulizi ya silaha za kemikali kaskazini mwa nchi hiyo.
Hadi hivi sasa Marekani inaendelea kulaaniwa kwa shambulio hilo la kivamizi ambalo limedharau sheria za kimataifa na ambalo halikusubiri hata kuanza uchunguzi kuhusu madai ya kutumiwa silaha za kemikali huko Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria.