Mar 16, 2023 04:15 UTC
  • Makabiliano ya kijeshi yasiyo ya kawaida kati ya Russia na Marekani katika anga ya Bahari Nyeusi

Kituo cha kamandi ya Marekani barani Ulaya kimetangaza kuwa Jumanne asubuhi, ndege ya kivita ya Russia aina ya Sukhoi Su-27 iligongana na ndege isiyo na rubani (droni) ya Marekani aina ya MQ-9 Reaper katika anga ya Bahari Nyeusi, na kupelekea droni hiyo kuanguka kwenye maji ya kimataifa.

Ndege mbili za kivita za Russia aina ya Sukhoi 27 ziliifutilia kwa karibu ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani katika hali ambayo Kamandi ya Ulaya ya Marekani ilikitaja kitendo hicho cha Russia kuwa "kisicho salama wala cha kitaalamu."

Katika taarifa ya kamandi hiyo, inadaiwa kuwa ndege ya Russia, pamoja na kuigonga ndege hiyo isiyo na rubani ya Marekani, iliinyunyizia mafuta na kuruka mbele yake kwa njia hatari na isiyo ya kitaalamu. Jenerali James B. Hacker, kamanda wa kituo hicho anadai kuwa droni hiyo ilikuwa inafanya operesheni za kawaida katika anga ya kimataifa ilipofuatiliwa na kisha kugongwa na ndege ya Russia. Anasema kugongwa huko ndiko kuliipelekea kuanguka na kisha kupotea kabisa.

Makabiliano ya ndege za Russia na Marekani katika Bahari Nyeusi

Uhusiano wa Russia na Marekani umeingia katika mkondo wa mivutano inayoongezeka kila siku hasa kufuatia hatua ya Marekani na washirika wake wa Ulaya ya kuipa Ukraine silaha za kisasa katika vita vyake na Russia. Msaada huo mkubwa pamoja na habari za kijasusi na kijeshi inazopewa Ukraine kutoka vituo vya kijeshi vya NATO na Marekani, habari ambazo bila shaka zinatolewa kupitia majukwaa mbalimbali ya kijasusi kama vile satelaiti, ndege za AWACS na bila shaka aina mbalimbali za ndege zisizo na rubani  za Marekani kama vile MQ9 Reaper, zimeiwezesha Ukraine kugundua na kufuatilia harakati za askari adui na kutoa mapigo kadhaa dhidi ya Russia katika mikoa tofauti ya Ukraine. Bila shaka Russia inafahamu vyema malengo ya harakati za ndege zisizo na rubani za Marekani katika eneo la Bahari Nyeusi na imekuwa ikiionya Washington mara kwa mara kuhusiana na suala hilo.

Tukio la shambulio la Jumanne katika anga ya Bahari Nyeusi linachukuliwa kuwa jambo muhimu na ambalo halijawahi kutokea katika muktadha wa makabiliano ya kijeshi kati ya Russia na Marekani. Bila shaka, Russia nayo tayari imetoa maelezo yake kuhusu tukio hilo ambapo kupitia taarifa iliyotolewa na wizara yake ya ulinzi siku ya Jumanne jioni, imesema ndege hiyo isiyo na rubani aina ya MQ9 ya Marekani ilikuwa ikiruka juu ya Bahari Nyeusi na karibu na peninsula ya Crimea, na kuwa ilikuwa ikiruka kuelekea kwenye mipaka ya Shirikisho la Russia. Imesema ndege hiyo ilikuwa ikiruka katika eneo hilo huku ikiwa imezima mitambo ya kuitambulisha, ambalo ni jambo hatari kiusalama na linalokiuka wazi sheria za kimataifa. Taarifa hiyo imeeleza kuwa hakuna silaha yoyote ya Russia iliyotumika kuitungua droni hiyo bali ilianguka yenyewe baada ya kupunguza masafa iliyokuwa ikitumia kuruka katika eneo hilo. Kwa msingi huo Moscow inakanusha kuhusika kivyo vyote vile katika kuiangusha ndege hiyo ya Marekani.

Anatoly Antonov

Hata hivyo, hatua hiyo ya Russia inachukuliwa kuwa onyo kali kwa Marekani kwamba iwapo itaendeleza operesheni zake za kijasusi katika eneo hilo kwa lengo la kuzituma kwa serikali ya Ukraine, bila shaka Moscow haitanyamazia kimya suala hilo bali itachukua hatua kali kukabiliana na vitisho vyo vyote vinavyokiuka usalama wake wa kitaifa na mistari yake miekundu. Kuhusiana na hilo, Anatoly Antonov, balozi wa Russia mjini Washington, amesema Moscow inaitaka Marekani kusimamisha mara moja harakati za ndege zake za kijasusi karibu na mipaka yake. Amesema John Kirby, ambaye ni msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani amesema safari za ndege za upelelezi za Marekani (kwenye mipaka ya Russia) ni shughuli ya kila siku; lakini anapasa kujibu swali hili kuwa je, ndege hizo zisizo na rubani zinafanya nini maelfu ya maili kutoka mipaka ya Marekani? Jibu liko wazi kabisa. Ndege zisizo na rubani za Kimarekani hukusanya habari ambazo serikali ya Kyiv huzitumia baadaye kushambulia vikosi vya jeshi la Russia na maeneo yaliyo chini ya mamlaka ya Russia.

Russia imeonya mara kwa mara juu ya uwepo wa vikosi vya kigeni katika maeneo yaliyo karibu na Ukraine pamoja na Bahari Nyeusi, na uwezekano wa kutokea makosa ya mahesabu ya kijeshi. Moscow imekuwa ikionya kwamba kutokana na mkondo wa matukio ya Ukraine, Russia na nchi za Magharibi tayari zimeingia katika vita vya niaba, na kwamba kuendelea kwa hali hiyo kunaweza kuibua vita vya moja kwa moja kati ya Russia na NATO.

Tags