Russia yailaumu Marekani kwa kukwamisha uchunguzi, Khan Shaykhun
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameeleza kusikitishwa na upinzani wa Marekani dhidi ya pendekezo lililotolewa na Moscow na Tehran kwa ajili ya kufanyika uchunguzi wa shambulizi la silaha za kemikali katika eneo la Khan Shaykhun nchini Syria.
Sergei Lavrov ameyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Marekani, Rex Tillerson na kukemea sana mwenendo huo wa Marekani.
Lavrov ameyasema hayo baada ya Shirika la Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) kukataa pendekezo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia la kundwa timu ya kufanya uchunguzi utakaobaini nani alifanya mashambulizi ya silaha za kemikali katika eneo la Khan Shaykhun nchini Syria. Zaidi ya watu mia moja waliuawa na wengine 400 kujeruhiwa katika shambulizi hilo.
Baada tu ya shambulizi hilo linalotia shaka, kambi ya nchi za Magharibi na za Kiarabu inayowaunga mkono magaidi nchini Syria ilifanya jitihada kubwa za kulihusisha shambulizi hilo la serikali ya Damascus, suala ambalo limekanushwa vikali na viongozi wa serikali ya Syria.
Shambulizi hilo pia limetumia na Marekani kama kisingizio cha kuhalalisha masmabulizi ya makombora ya nchi hiyo dhidi ya kituo cha anga chaShayrat katika mkoa wa Homs nchini Syria tena bila ya idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.