May 02, 2017 04:05 UTC
  • Majeshi ya Iran,  Syria kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi

Wakuu wa majeshi ya Iran na Syria wamesisitiza kuhusu kuimarisha ushirikiano wa majeshi ya nchi mbili katika vita dhidi ya ugaidi huku wakilaani vikali hujuma za Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Syria.

Meja Jenerali Mohammad Baqeri Mkuu wa Majeshi Yote ya Iran na mwenzake  wa Syria Jenerali Ali Abdullah Ayoub, wameyasema hayo katika mazungumzo yao mjini Tehran siku ya Jumatatu.

Meja Jenerali Baqeri amepongeza mapambano ya kishujaa ya watu na Jeshi la Syria mbele ya jinai za magaidi wakufurishaji na hujuma za madola ya kigeni.  Aidha amelipongeza jeshi la Syria na vikosi vya kujitolea vya wananchi kufuatia ushindi wao katika kuukomboa mji wa Aleppo na pia kuwaokoa wakaazi waliokuwa wamedhulumiwa na kuzingirwa na magaidi katika vijiji vya Fua'a na Kefraya.

Aidha mkuu wa majeshi ya Iran amelaani vikali hujuma za anga za ndege za kivita za Marekani na Utawala Haramu wa Israel nchini Syria na kusema: "Watu wa Syria kwa kulinda umoja na mshikamano wa kitaifa sambamba na kufanya mazungumzo baina yao wanapaswa kuchukua tahadhari kuhusu njama za maadui wa kigeni wanaolenga kuibua mifarakano nchini humo."

Meja Jenerali Mohammad Baqeri wa Iran (kulia)  na Brigedia Ali Abdullah Ayoub wa Syria

Kwa upande wake Jenerali Ayoub, Mkuu wa Majeshi Yote ya Syria katika kikao hicho amewasilisha ripoti ya matukio ya hivi karibuni katika medani ya vita Syria hasa vita dhidi ya magaidi wakufurishaji. Aidha amesema uhusiano wa Iran na Syria katika sekta za siasa na kijeshi ni mzuri. Ameongeza kuwa,  sera zenye busara za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuunga mkono amani na uthabiti katika eneo na ulimwengu wa Kiislamu sambamba na kuheshimu mamlaka ya kujitawala nchi za eneo ni jambo linalopongezwa na nchi huru na wapenda uhuru duniani. Mkuu wa Majeshi Yote ya Syria aliwasili  Iran Jumatatu akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kijeshi kufuatia mwaliko wa mwenzake wa Iran.

Tags