Wahajiri 7 wafa maji, 484 waokolewa katika bahari ya Mediterania
Gadi ya Pwani ya Italia imesema wahajiri saba wamepoteza maisha huku wengine zaidi ya 400 wakiokolewa katika bahari ya Mediterania wakijaribu kuelekea barani Ulaya jana Jumamosi.
Taarifa ya gadi hiyo iliyonukuliwa na shirika la habari la Reuters imesema wahajiri 484 walikolewa wakiwa katika boti nne za mipira na timu ya wapiga mbizi wa Italia na meli mbili za kibinfasi.
Hata hivyo taarifa ya Gadi ya Pwani ya Italia haijatoa maelezo zaidi kuhusu ajali hiyo ya boti na asili ya wahajiri waliokuwa katika boti hizo.
Wiki iliyopita, Gadi ya Pwani ya Italia ilisema wahajiri elfu 6 wameokolewa katika kipindi cha siku mbili zilizopita katika bahari ya Mediterania wakijaribu kuelekea barani Ulaya.
Wahajiri 45,000 wamewasili Italia kwa boti hafifu za plastiki wakitokea kaskazini mwa Afrika tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa huku wengine zaidi ya 1,222 wakiaga dunia kwa kuzama baharini, hili likiwa ni ongezeko la asilimia 40 ya vifo vya wahajiri wanaoelekea Italia, ikilinganishwa na mwaka jana 2016.
Mwaka jana wahajiri zaidi ya 5000 hususan wa Kiafrika walipoteza maisha kwa kuzama baharini katika bahari ya Mediterania wakiwa katika safari hizo hatari za kuelekea Ulaya.