Watu 20 wauawa katika mlipuko mazikoni Kabul, Afghanistan
Watu wasiopungua 20 wameuawa katika mlipuko wa kigaidi wakiwa katika maziko katika kitongoji cha mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.
Kwa mujibu wa mwandishi wa Radio Tehran mjini Kabul, alasiri ya leo, watu 20 wameuawa kufuatia milipuko mitatu katika eneo la Khair Khana wakati wa mazishi ya Mohammad Salim Ezadyar, mwana wa Mohammad Alam Ezadyar, Naibu Spika wa Bunge la Senate nchini Afghanistan.
Salim aliuawa Ijumaa wakati wa mapambano baina ya polisi na waandamanaji mjini Kabul.
Hadi sasa hakuna kundi au mtu yeyote aliyetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi. Maandamano hayo yalikuwa yameitishwa kuitaka serikali iimarishe usalama baada ya watu 100 kuuawa na wengine 500 kujeruhiwa katika hujuma ya kigaidi.
Maafisa wa usalama Afghanistan wanadai kundi la kigaidi la Haqqani na Shirika la Kijasusi la Jeshi la Pakistan ISI ndio wahusika wa hujuma hiyo. Hata hivyo Pakistan imekanusha madai hayo huku kundi la kigaidi la ISIS au Daesh likidai kuhusika na hujuma hiyo ya Jumatano mjini Kabul.