Waislamu Uingereza walaani mashambulizi ya kigaidi London, Manchester
Waislamu nchini Uingereza wamelaani vikali mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni katika miji ya London na Manchester yaliyosababisha vifo vya makumi ya watu.
Taarifa iliyotolewa na viongozi 130 wa Kiislamu nchini humo imesema kuwa, mashambulizi hayo ya kigaidi yamekosa kufikia malengo yake ya kuwagawanya Waingereza kwa misingi ya kidini.
Wamesema: "Kwa mara nyingine tena wimbi la mashambulizi ya kigaidi limeikumba nchi hii, hujuma ambazo zimefanywa na makatili wanaotaka kuhalalisha jinai zao nyuma ya pazia la dini. Tunataka kusisitiza kuwa, vitendo hivyo havina baraka wala uhusiano wowote na dini yetu tukufu."
Taarifa ya viongozi wa Kiislamu nchini Uingereza imebainisha kuwa, katika hali ambayo Waislamu kote duniani wanajipinda na kufanya jitihada za kukithirisha ibada zao kwa lengo la kufikia upeo wa ucha-Mungu katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, magaidi hao wanaojiita Waislamu wanashadidisha harakati zao zisizo na utu wala dini.
Kadhalika wametangaza kuwa hawatowaswalia magaidi waliouawa katika hujuma ya hivi karibuni ya London kwa kuwa waliuawa wakijaribu kuuchafua utambulisho halisi wa Uislamu.
Jumamosi usiku, magaidi hao watatu waliua watu saba katika tukio lililohusisha watu kugongwa na gari na wengine kuchomwa visu katika eneo la Daraja la London. Tukio hilo limetokea majuma kadhaa tu baada ya watu 22 kuuliwa pale mhanga mmoja wa kujitolea kufa, alipojilipua ndani ya uwanja mmoja wa burudani huko mjini Manchester.