Waliouawa kwa maporomoko ya ardhi Bangladesh wapindukia 130
Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na maporomoko ya ardhi nchini Bangladesh imepindukia watu 130.
Duru za polisi, jeshi na wazima moto wanaohusika na shughuli za kuwaokoa wahanga wa janga hilo zinasema watu 132 wamethibitishwa kupoteza maisha kufikia Jumatano hii nchini humo, hususan katika wilaya za kusini mashariki mwa nchi.
Reaz Ahmed, afisa wa ngazi za juu katika Idara ya Kukabiliana na Majanga ya Bangladesh mapema leo amesema maporomoko hayo ya ardhi yamesababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo; na kwamba watu 98 wameaga dunia kutokana na maporomoko hayo katika wilaya ya Rangamati, 28 katika wilaya ya Chittagong na wengine sita katika wilaya ya Bandarban.
Naye Rezaul Karim, msemaji wa jeshi la nchi hiyo amesema askari jeshi ni miongoni mwa watu walipoteza maisha katika janga hilo la kimaumbile na kwamba nyumba zaidi ya 5000 zimebomolewa na maporomoko hayo.
Mapema mwezi huu, kimbunga kikali kinachoitwa Mura, kilipelekea zaidi ya watu laki tano kuyahama makazi yao nchini Bangladesh.
Taarifa kutoka nchini Bangladesh zinaarifu kwamba, familia za wakimbizi Waislamu wa Rohingya zinakabiliwa na hali mbaya sana kufuatia maeneo wanayoishi kukumbwa na kimbunga hicho na maporomoko ya ardhi.