Waislamu walioshiriki mazishi ya binti aliyeuawa Marekani walaani ubaguzi dhidi yao
https://parstoday.ir/sw/news/world-i30828-waislamu_walioshiriki_mazishi_ya_binti_aliyeuawa_marekani_walaani_ubaguzi_dhidi_yao
Waislamu walioshiriki mazishi ya binti wa Kiislamu aliyeuawa siku chache zilizopita na kijana mwenye chuki dhidi ya Uislamu huko katika jimbo la Virginia nchini Marekani, wamelaani vikali ongezeko la ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 22, 2017 09:47 UTC
  • Waislamu walioshiriki mazishi ya binti aliyeuawa Marekani walaani ubaguzi dhidi yao

Waislamu walioshiriki mazishi ya binti wa Kiislamu aliyeuawa siku chache zilizopita na kijana mwenye chuki dhidi ya Uislamu huko katika jimbo la Virginia nchini Marekani, wamelaani vikali ongezeko la ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.

Mazishi ya mwili wa Nabra Hassanen aliyeuawa Jumapili iliyopita yamehudhuriwa na mamia ya Waislamu wanaoishi nchini Marekani ambapo wameonyesha hasira zao juu ya vitendo vya ukatili na ubaguzi wa kupindukia dhidi yao tangu ilipongia madarakani serikali ya sasa chini ya Rais Donald Trump wa nchi hiyo.

Familia ya marehemu Nabra Hassanen ikiwa na majonzi

Hii ni katika hali ambayo polisi ya Marekani imejaribu kutoyahusisha mauaji hayo dhidi ya binti huyo wa Kiislamu aliyekuwa na umri wa miaka 17 na chuki za kidini au ubaguzi. Aidha mbali na mazishi ya mwili wa Nabra Hassanen kuhudhuriwa na Waislamu, shakhsia na viongozi wa mji wa Virginia akiwemo kamanda wa polisi wa eneo la Sterling, maimamu wa misikiti na viongozi wa dini za Kiyahudi na Kikristo kutoka maeneo tofauti ya Marekani wamehudhuria mazishi hayo. 

Ndugu na jamaa wakitoa salamu na heshima zao kwa mwenda zake Nabra Hassanen

Nabra Hassanen, aliuawa siku ya Jumapili iliyopita baada ya kutoka msikitini katika jimbo hilo ambapo alitekwa nyara na kupigwa na mtu mwenye chuki za kidini jimboni hapo. Inaelezwa kuwa, akiwa pamoja na marafiki zake wakitoka msikitini, kijana huyo mwenye chuki za kidini alianza kuwashambulia kwa matusi machafu ambapo katika kujibizana kwa maneno, kijana huyo alishuka kutoka kwenye gari lake na kuanza kumpiga na kisha kumteka nyara Nabra na kwenda naye kusikojulikana, huku mwili wa wake ukiokotwa katika bwawa la maji eneo la Sterling mita kadhaa kutoka eneo la tukio hilo.

Msafara uliobeba mwili wa Nabra

 Polisi walitangaza kumtia mbaroni kijana huyo anayejulikana kwa jina la Darwin Martinez Torres mwenye umri wa miaka 22.